*Aiagiza TFS kuyapiga mnada magogo yaliyovunwa kinyume cha utaratibu

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Paul Matiko kusimamia ujenzi wa kituo cha Afya Usinge na kuhakikisha kinakamilika ifikapo Oktoba 2021 ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma za afya.

 

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Agosti 28, 2021) alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kilitengewa shilingi milioni 620 za ujenzi.

 

Waziri Mkuu amesema kuwa amefika katika eneo la kituo hicho lakini hajaona vifaa vya ujenzi ambavyo awali aliambiwa vimenunuliwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi ikiwa tayari zimeshatumika shilingi milioni 600 lakini vifaa hivyo havipo eneo la ujenzi na kiasi hicho cha fedha kilitakiwa tayari kiwe kimekamilisha ujenzi huo.

 

“Sitawaelewa mkiniambia mnatafuta fedha nyingine na kuzileta hapa ili muongeze kwenye milioni 620 kukamilisha ujenzi wa majengo katika kituo hiki, na hili watu mjiande, Serikali yetu ipo makini na usimamizi wa fedha za serikali upo vilevile”

 

Amesema kuwa ukamilikaji wa kituo hicho cha Usinge kitakuwa mkombozi kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuwa kitawafanya kutokusafiri umbali mrefu hadi Kaliua kufuata huduma za afya kwa kuwa kituo hicho kitakuwa na huduma zote muhimu.

 

“Mheshimiwa Rais, ameleta kwenye Wilaya yenu Bilioni 1 na Milioni 860 kwa ajili ya dawa, na kila mwezi Halmashauri inapokea fedha Shilingi Milioni 165, Mna vituo vya afya na Zahanati, nisisikie vituo hivyo vinakosa dawa, Madiwani naomba msimamie katika vituo hivyo kusiwe na mapungufu”

 

Katika Hatua nyingine, Waziri Mkuu alitembelea eneo la pori la akiba la Igombe na kushuhudia magogo yaliyokamatwa baada ya kukatwa kwa njia haramu na ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuyapiga mnada magogo hayo kwa kufuata utaratibu.

 

“Wizara toeni vibali vya mnada magogo haya yauzwe, na yaliyo humo ndani hifadhini TFS nendeni mkayakusanye haraka sana ili mpaka mwishoni mwa mwezi wa tisa yawe yamekusanywa na kuuzwa kupitia mnada, waambieni wanunuzi mtayapiga mnada lini ili waje hapa kila mtu ajaribu bahati yake”

 

Aidha, Waziri Mkuu ameagiza Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuhakikisha wanaongeza ulinzi katika eneo la hifadhi hiyo ili kuwalinda wanyama wanaokatiza na wasisite kuwachukulia hatua kali wale watakaokamatwa wakifanya ujangili.

 

“Hawa lazima tuwafanyie msako tuwakamate, awe anatoka Tanzania au nje ya nchi, ana silaha, kamata aingie kwenye mkono wa sheria, tengeneza timu yako upekuzi ufanyike”

 

Akiongea na Wanakijiji cha Wachawaseme, Kaliua mkoani Tabora, Waziri Mkuu amewasihi kuulinda msitu ulio katika pori la akiba la Igombe kwa kuacha kukata miti ili kulinda uoto katika eneo hilo

 

“Tunaharibu miti, hili bonde lote ni eneo linalosaidia kutoa maji kwenda mto Malagarasi lakini pia ziwa Tanganyika, mkiacha miti iondolewe eneo hili litakuwa kavu na hakutakuwa na maji, hapa ni nyumbani kwenu, ni wajibu wenu kulinda maliasili hii”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...