Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
WAUMINI wa Kanisa la Baptist Kinondoni mkoani Dar es Salaam wakiongozwa na Mchungaji wa kanisa hilo Samweli Kabonaki wamefanya ibada maalum ya kuliombea Taifa la Tanzania katika kipindi hiki cha janga la Corona.
Akizungumza wakati wa Ibada hiyo ,Mchungaji Kabonaki amesema Watanzania na Dunia wanajua kipindi tunachopitia kutokana na uwepo wa janga la Corona ambalo limeleta madhara katika mataifa mbalimbali,hivyo wameona ni vema Kanisa hilo likafanya maombi maalum kuliombea taifa la Tanzania.
Amesema kwamba katika kukabiliana na janga la Corona pamoja na hatua ambazo zinachukuliwa, ni vema kila mmoja wetu akamtanguliza Mungu zaidi na yvema ikajulikana Mungu ndiye mwenye majibu yote na ni mponyaji mkuu.
Amefafanua hilo kwa kunukuu maandiko matakatifu kutoka Neno lilitoka 1 Wafalme 18:35-40 na ijulikane kwamba katika Tanzania kuna Mungu wa pekee ndiye Mungu aponyaye.
Katika hatua nyingine Mchungaji Kabonaki amewaomba waumini wa kanisa hilo wafuate maelekezo kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na watalaam wa afya kuhakikisha kila mmoja anajikinga na kumkinga mwingine dhidi ya maambukizi ya Corona.
"Watumishi wa Mungu tunalo jukumu la kuliombea Taifa na watu wake wakiwemo viongozi wetu, lakini kwa nafasi ya kila mmoja wetu tunatakiwa kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali kupitia watalaam wake wa afya,"amesema Mchungaji Kabonaki.
Amesisitiza kuwa utawala wa Awamu ya Sita umekuwa ukimtanguliza Mungu mbele ,hivyo amewaomba Watanzania kuendele kuwaombea viongozi wote ili watekeleze majukumu yao licha ya kuwepo kwa vikwazo mbalimbali.
Mchungaji Kabonaki pia amewaomba waumini wa dini ya Kikristo kuwa mfano wa kuigwa katika utunzaji wa mazingira kwani bila kuwepo kwa mazingira safi magonjwa yatapata nafasi katika jamii."Kwa nafasi yetu tutahakikisha tunaendelea kufanya Maombi kuiombea Serikali ya Awamu ya Sita na viongozi wake."
Pia amewaomba wananchi wote kuhakikisha hawawapi nafasi watu ambao wamekuwa na roho za uadui,kusema vibaya na kukatisha tamaa wengine."Tusivunjike moyo kwa maneno ya watu wenye roho za uadui,chuki,usenganyaji na wenye kukatisha tamaa.Sisi sote tujikite kufanya kazi kwa maendeleo ya nchi yetu."
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...