Na Muhidin Amri,Tunduru
WAKULIMA wa mbaazi katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wameendelea
kuvuna fedha kufuatia kupanda kwa bei ya zao hilo kutoka shilingi 1,294
katika mnada wa kwanza hadi shilingi 1,428 mnada wa tatu.
Wakizungumza, wakati wa mnada wa tatu uliofanyika katika kijiji cha
Lukumbule wilayani humo,baadhi ya wakulima wamefurahi mfumo wa
stakabadhi ghalani ambao umewezesha kupanda kwa bei ya mbaazi kwa kila
mnada.
Hadija Mitete amesema, kabla ya zao hilo kuingizwa katika mfumo wa
stakabadhi ghalani hawakuwa na manufaa yoyote licha ya kutumia nguvu
kubwa katika uzalishaji kutokana na wafanyabiashara kununua mbaazi kwa
bei ndogo tofauti na sasa tangu Serikali ilipoanzisha mfumo wa
stakabadhi ghalani.
Ameipongeza Serikali kwa kusimamia mfumo huo, ambao umewasaidia
kumaliza unyonge wa muda mrefu wa kukosa soko la uhakika wa zao hilo
ikilinganisha na wakulima wa mazao mengine.
Hata hivyo,amewaomba wanunuzi kulipa fedha kwa wakati ili ziwasaidie
kusomesha watoto na kununua pembejeo za kilimo hususani dawa(Salphur)kwa
ajili ya kupulizia korosho.
Daimu Kalambo amesema, mfumo wa stakabadhi ghalani ni nzuri kwa kuwa
umeleta tija kwa wakulima kwa kupata bei kubwa ya mazao yao tofauti na
soko hulia ambapo wafanyabiashara walinunua mazao kwa bei wanayopanga
wao jambo lililosababisha umaskini mkubwa kwa wakulima.
Ameiomba Serikali, kuendelea kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani hata
kwa mazao mengine ya biashara ikiwemo mpunga ili kuwasaidia wakulima
kupata soko la uhakika na bei nzuri.Kwa upande wake Afisa Ushirika wa wilaya ya Tunduru George Bisani
amesema, katika mnada huo jumla ya kilo 1,324.886 zimeingizwa mnadani
na wanunuzi saba walijitokeza katika mnada huo.
Bisani amesema, kampuni ya Export Trading Co Ltd imeshinda ambayo
imenunua mbaazi zote kwa bei ya Sh.1,428 kwa kilo moja na kufanya jumla
ya Sh. 1,891,937,208.00 kuingia katika mzunguko wa fedha katika wilaya
ya Tunduru kupitia zao la mbaazi.
Amesema, mpaka sasa mwenendo wa minada ni nzuri kwa bei ya mbaazi
inaendelea kupanda tokea mnada wa kwanza ambayo ilikuwa Sh 1,294 kwa
kilo moja.
Kwa mujibu wa Bisani,katika mnada wa pili bei ilikuwa Sh 1,341 kwa kilo
moja ikiwa ni ongezeko la Sh. 47 na katika mnada wa tatu bei imefikia Sh
1,428 sawa na ongezeko la Sh 87.
Bisani, amewashukuru wakulima wote ambao wameamua kupeleka mazao yao
kwenye Vyama vya msingi ili wakutanishwe na wanunuzi wenye bei ya
juu(kubwa) ambayo itahamasisha wakulima wengi zaidi kupeleka mbaazi zao
kwenye vyama vya ushirika na kuongeza uzalishaji katika msimu ujao.
Amewatoa hofu wakulima juu ya kukosekana kwa vifungashio(mifuko) na
kusema kuwa,tayari Serikali kupitia Chama Kikuu cha Ushirika imeshaleta
kwa wingi na vinatosheleza mahitaji ya wakulima wa zao hilo.
Aidha amesema kuwa,malipo ya wakulima waliopeleka mbaazi katika mnada
wa tatu wataingiziwa fedha kwenye akaunti zao ndani ya siku saba tokea
siku ya mnada.
Akifunga mnada huo, Kaimu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika
wilayani humo(Tamcu Ltd) Pino Chikojola, ameishukuru Serikali kwa
kuwadhibiti wanunuzi na walanguzi holela wa mazao ambao wanapenda wapate
faida kubwa na kumuacha mkulima akiendelea na umaskini.
Amesema, mfumo wa stakabadhi ghalani katika wilaya ya Tunduru umewezesha kupandisha uzalishaji na thamani ya mazao yao.
Amewataka wakulima kujitahidi kulima mazao mbalimbali ya chakula na
biashara ili kutatua changamoto ya umskini kwenye kaya zao kwa kuwa
Serikali imeonesha dhamira ya kuwasaidia wakulima.
Baadhi ya wakulima na wananchi wa kijiji cha Lukumbule wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakimsikiliza jana Afisa Ushirika wa wilaya hiyo George Bisani(hayupo pichani)wakati wa mnada wa tatu wa zao la mbaazi zinazouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani. Picha zote na Muhidin Amri,
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...