Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

MCHEZAJI wa Kimataifa wa Msumbiji na Klabu ya Simba ya Tanzania, Luis Jose Miquissone ametajwa kutimkia katika Klabu ya Al Ahly ya Misri baada ya timu hiyo kufika makubaliano na Simba SC katika uhamisho huo uliotajwa kufikia Shilingi Bilioni 2 za Kitanzania.

Taarifa za Simba SC kumalizana na Al Ahly SC katika uhamisho huo wa Miquissone zimekuja baada ya Mwandishi wa Habari za Michezo kutoka Ghana, Nuhu Adams kueleza kupitia Mitandao yake ya Kijamii kuhusiana na uhamisho wa Mchezaji huyo machachari.

Mwandishi huyo maarufu na Mchambuzi wa masuala ya Michezo nchini Ghana ameeleza, “Ni rasmi Al Ahly SC na Simba SC zimefika makubaliano ya uhamisho wa Nyota wa Kimataifa wa Mozambique, Luis Jose Miquissone (26) kwa ada ya US$900,000”.

Luis Miquissone maarufu Konde Boy hapa nchini amekuwa tishio kwa vilabu mbalimbali katika mashindano mbalimbali hadi kuwavutia matajiri wa Soka barani Afrika, National Al Ahly ambao ni Mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL) walimuona Miquissone kwenye msimu huu Ligi ya Mabingwa Afrika akiwasumbua mara kadhaa wao sambamba na timu mbalimbali zilizoshiriki Michuano hiyo.

Miquissone amewahi kuwafunga Al Ahly SC wakati Simba SC ikipata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Hatua hiyo ya kusajiliwa kwake kwa Mabingwa hao ni imeelezwa pendekezo la Kocha Mkuu wa Al Ahly, Pitso Mosimane baada ya kuvutiwa na kiwango chake.

Al Ahly SC timu bora na Mabingwa wa Afrika mara mbili mfululizo katika misimu ya 2019-2020 wakizifunga timu maarufu na ngumu katika mpira wa Afrika. Msimu wa 2019-2020 kwenye Fainali ya CAF CL waliwafunga Zamalek 2-1 katika dimba la Cairo International nchini Misri.

Msimu wa 2020-2021 katika mchezo wa Fainali, Al Ahly SC waliwafunga Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini bao 3-0 katika mchezo wa Fainali uliopigwa kwenye dimba la Mohammed V nchini Morocco.

Luis Miquissone alisajiliwa Simba SC Januari 2020 akitokea Klabu ya UD Songo ya Msumbiji ikiwa ni baada ya timu hiyo kuisumbua Simba SC ya Patrick Aussems katika Michuano ya CAF CL msimu wa 2019-2020.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...