Benki ya NMB, imesaini makubaliano ya ushirikiano na Hospitali ya CCBRT, yanayolenga kukusanya kiasi cha Sh. Bilioni 1 za matibabu ya Fistula kwa kina mama wasio na uwezo, kupitia Mbio za Hisani za NMB Marathon, zitakazofanyika kwa mara ya kwanza Septemba 18, 2021 jijini Dar es Salaam.

 Kupitia mbio hizo ambazo mwaka huu zitafanyika chini ya kaulimbiu ya: 'Mwendo wa Upendo,' Benki ya NMB na CCBRT wanatarajia kukusanya zaidi ya Sh. Milioni 250 kila mwaka kwa miaka minne ambazo zitasaidia matibabu ya wagonjwa wa fistula, miongoni mwa mamia ya kina mama wanaoteseka kwa maradhi hayo.

 Akizungumza wakati wa utilianaji saini wa makubaliano hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alibainisha kuwa, Fistula ni maradhi yanayotesa kina mama wengi nchini, na akawataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujisajili kushiriki mbio hizo, ili kufanikisha lengo la kukusanya fedha ya matibabu ya wagonjwa hao.

 Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi, alisema taasisi yake inajisikia faraja kubwa kufanikisha utilianaji saini wa makubaliano hayo, sambamba na uzinduzi wa NMB Marathon 2021, huku akieleza kuwa mashindano hayo yana maana kubwa kwa maelfu ya kina mama wa Kitanzania.

 NMB Marathon zitakuwa na sehemu tatu ambazo ni mbio za kilomita 21 (nusu marathon), kilomita 10 na kilomita 5, ambako washindi wa kwanza hadi wa 10 watapata medali na fedha taslimu.

 Kwa mujibu wa Mratibu wa NMB Marathon 2021, David Marealle, ada ya kujisajili kushiriki mbio hizo ni Sh. 30,000 kwa kilomita 21 na Sh. 20,000 kwa mbio za kilomita 10 na kilomita 5.

 Washindi wa mbio za kilomita 21 wanaume na wanawake watajinyakulia Medali ya Dhahabu na fedha taslimu Sh. 1,400,000, huku washindi wa pili wakitarajiwa kutwaa Medali za Fedha na Sh. 1,100,000, wakati washindi wa tatu wakitengewa Sh. 700,000 na Medali za Shaba.

 Huku kwa mbio za kilomita kumi, 700,000 na medali ya dhahabu, 500,000 na medali ya fedha pamoja na 300,000 na medali ya Shaba kwa mshindi wa kwanza, pili na tatu kwa wanaume na wanawake.

 Katika mbio za kilomita 5, washindi upande wa wanawake na wanaume watajipoza na Medali za dhahabu na Sh. 250,000, washindi wa pili medali za fedha na Sh. 150,000, huku washindi wa tatu wakiambulia medali za shaba na Sh. 100,000 taslimu.

Tayari kampuni za Bima za UAP na SANLAM wameshachangia jumla ya shilingi milioni 100 (sawa na Sh. Mil. 50 kila moja)

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki y NMB, Ruth Zaipuna na Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi  wakionyesha mkataba  wa maelewano baada ya kutiliana saini mkataba wa maelewano wa mbio za NMB Marathon zenye lengo la kuchangia bilioni mmoja ndani ya miaka minne kwa ajili ya kuwatibu akinamama wenye Fistula. Kulia ni  Afisa Mtendaji Mkuu wa UAP Insurance, Nelson  Rwihula na kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Sanlam Life Insurance,  Julius Magabe. 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki y NMB, Ruth Zaipuna na Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi wakibadilishana  wa maelewano wa mbio za NMB Marathon zenye lengo lakuchangia bilioni mmoja ndani ya miaka minne kwa ajili ya kuwatibu akinamama wenye Fistula. Kulia ni  Afisa Mtendaji Mkuu wa UAP Insurance, Nelson Rwihula na kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Sanlam Life Insurance, Julius Magabe 

 


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...