Na Karama Kenyunko Michuzi TV

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa Mwenyekiti wa  Chadema, Freeman Mbowe, aliomba kutafutiwa Makomandoo wanajeshi waliofukuzwa kazi au wastaafu, ili awatumie katika kuwadhuru viongozi wa serikali akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha Lengai Ole Sabaya.

Hayo yameelezwa leo Agosti 23,2021 wakati upande wa Jamuhuri ulipokuwa ukiwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Wakili wa serikali Mwandamizi Nassoro Katuga akisoma maelezo ya shahidi wa Jamuhuri kutoka JWTZ, Luteni Denis Urio amedai, (Luteni) alifahamiana na Mbowe Mikocheni 2012 ambapo alimueleza harakati za ukombozi wa nchi alizokuwa nazo.

Amedai katika maongezi yao, Mbowe alimueleza amtafutie kampuni ya kufunga mitambo lakini yeye akamwambia jeshini wataalamu hao hawapo hivyo atafute maeneo mengine.

Akadai, Juni 2020 Mbowe alimpigia tena simu akitaka wakutane lakini yeye akasema hana nafasi na kumtaka waongee kwa simu lakini Mbowe alikataa akasema waonane kwa kuwa maongezi hayo hayafai kuongelewa kwenye simu.

Akadai kuanzia hapo Mbowe hakumtafuta tena hadi Julai 2020 ambapo yeye (Luteni) alimtafuta Mbowe akamwambia waonane, wakakutana Mikocheni.

Akadai walipokutana huko akamwambia chama cha Chadema kitachukua dola na yeye (Luteni) angepewa nafasi ya juu hivyo amtafutie hao wanajeshi ili wamsaidie  katika harakati za kuchukua dola na kumtuliza Sabaya kwa kumshikisha adabu na si kumuua kwa sababu taarifa za mbowe kunyanyaswa na Sabaya ameishazifikisha kwa Rais na kwa IGP bila mafanikio.

Anadai alimpigia simu mkurugenzi wa makosa ya jinai DCI Robert Boaz akamsimulia kila kitu alichoambiwa na Mbowe Boaz akamwambia kila hatua itakayokuwa inaendelea amtaarifu ASP Kingai.

Akiendelea kusoma maelezo ya Luteni Urio, Katuga akadai, Mbowe alimtumia sh. laki tano Luteni kwa kutumia simu yake na Luteni nae akatoa laki tatu akampa Halfani Bwire, ikabakia 195,000 katika simu yake Mbowe akamtumia tena Luteni 199,000. Baada ya kupata vijana hao Mbowe hakumtafuta tena Luteni akakata mawasiliano badala yake Luteni akawa anawasiliana na Bwire kuhusiana na matukio yote yaliyokuwa yakiendelea ...

Akisoma maelezo ya DCI Boaz amedai, mwezi Julai 2020 Kamishna wa polisi Robert boaz alipokea simu akiwa Dar es Salaam kutoka kwa mtu asiyemjua akamwambia kuna uhalifu unapangwa kufanyika kwa ajili ya kuwadhuru viongozi wa serikali.

Anasema mtu huyo alijitambulisha kuwa yeye ni Luteni mstaafu wa JWTZ Denis Urio. Akamwambia aende ofisini kwake ambapo alipoenda akamwambia Mbowe alimpigia simu anataka amtafutie wanajeshi wastaafu au waliofukuzwa kazi, na makomandoo au ili kuwadhuru viongozi akiwemo Sabaya lengo likiwa nchi isitawalike, wataka miti, magogo na watalipua vituo vya mafuta. 

Boazi akamwambia Luteni asijitoe  katika mpango huo endelea kumtafutia watu hao anaowataka, Urio alimtafutia watu wawili walioshiriki mpango wa kumdhuru Sabaya mpango ambao ulikamilika.

Akadai ulipofanywa na jeshi la polisi Upelelezi kuhusu uhusika wa Mbowe wakabaini kuwa yeye (Mbowe) ndio kinara.

Akisoma maelezo ya Mrakibu Msaidizi wa Polisi Ramadhani Kingai, Katuga amedai siku hiyo alikuwa katika kituo chake cha kazi mkoani Arusha, ambapo aliitwa na DCI Boaz kwa ajili ya kwenda kumsililiza Luteni Urio, ambapo nae alimsimulia kitu kile kile kuhusu Mbowe kutaka kufanya vitendo vya kigaidi na kumueleza kuwa kati ya vijana hao watatu aliotafutiwa mmoja wapo Mbowe alimgeuza kuwa mlinzi wake.

Akadai, Agosti 4, 2020 majira ya mchana, vijana watatu waliotafutwa walienda kwa Mbowe Moshi kwa ajili ya mkakati wa kumdhuru Sabaya ndipo askari watatu waliwafuatilia na kuwakuta Grocery ambapo walifanyiwa upekuzi.

Akadai Agosti 6, 2020 watuhumiwa hao watatu walitolewa mahabusu kwenda kumtafutia mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Moses lakini hawakumpata ndipo wakawachukua watuhumiwa na kuwaleta Dar es s Salaam na kufika Agosti 7, 2021

Katika maelezo ya SP Jumanne amedai , pamoja na mambo mengine, alipewa jukumu la kwenda kumuhoji Mbowe kwa ajili ya kutoa maelezo akasema hawezi kuongea bila ya kuwepo kwa wakili wake, lakini hata alipokuja wakili wake Fredrick Kihwelo, Mbowe alidai kuwa atatoa maelezo mahakamani.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...