WIZARA ya Mifugo na Uvuvi kupitia sekta yake ya Mifugo ipo mbioni kununua kiwango kikubwa cha gesi aina ya “liquid nitrogen” kutoka kiwanda cha kutengenezea gesi hiyo kinachojulikana kama “Tanzania Oxygen Limited” (TOL) kilichopo Mkoani Dar-es-salaam.

Hayo yamesemwa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Mifugo) Dk Bedan Masuruli mara baada ya kutembelea kiwandani hapo ili kukagua uwezo wa kuzalisha gesi hiyo ambapo ameridhishwa na kiwango cha uzalishaji kilichopo na kuahidi kuanza mchakato wa taratibu za manunuzi ya gesi hiyo.

“Waziri wetu Mashimba Ndaki ametuagiza tuhakikishe tunahimilisha ng’ombe milioni 5 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa na jambo hilo haliwezi kufanikiwa kama hatutakuwa na uhakika wa upatikanaji wa gesi hii kwa sababu ndio inayotumika kuhifadhi mbegu hivyo baada ya kuwatembelea leo tumeridhika na kiwango chao cha uzalishaji na tuna uhakika kiwango hiki kitatusaidia kufikisha lengo letu” Amesema Dk Masuruli.

Dk Masuruli ameongeza kuwa lengo la Wizara hiyo ni kuhakikisha inazalisha mbegu bora za ng’ombe wa nyama na maziwa kupitia teknolojia ya uhimilishaji ambapo amewataka wafugaji watarajie kuanza kupata mbegu hizo ili waweze kufanya shughuli yao ya ufugaji kwa tija.

Akibainisha mabadiliko chanya yatakayopatikana baada ya kuanza matumizi ya gesi kutoka kiwandani hapo, Meneja wa kituo cha Uhimilishaji cha Sao-Hill kilichopo Mji mdogo wa Mafinga, Thomas Tegulo amesema kuwa itawasaidia kuhimilisha ng’ombe wengi zaidi tofauti na ilivyo hivi sasa kutokana na mitambo ya kutengenezea gesi hiyo iliyopo kituoni hapo kuharibika.

“Mtambo wetu wa kuzalisha gesi ya “liquid Nitrogen” umeharibika kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa hivyo tumefarijika kuona kiwango kikubwa cha uzalishaji wa gesi hiyo kilichopo hapa ambapo sasa tuna uhakika tutazalisha mitamba bora mingi zaidi” Amesema Tegulo.

Naye Mkurugenzi wa Masoko na biashara wa kiwanda hicho Mhandisi Daudi Mlwale amesema kuwa kiwanda chao kimesimika mtambo mkubwa zaidi wa kuzalisha gesi hiyo ambao una uwezo wa kuzalisha wastani wa lita 7200 za gesi hiyo kwa siku.

“Ni faraja kwetu kuona Wizara na Serikali kwa ujumla imeona upo umuhimu wa kununua gesi inayozalishwa hapa nchini na sisi tunawakaribisha na kuahidi kufanya nao kazi kwa sababu uwezo upo na nia ipo kwa hiyo ni suala tu la kukamilisha taratibu chache ili tuweze kuzalisha na kuwapatia” Ameongeza Mhandisi Mlwale.

Kwa kipindi cha miaka mitano ijayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia sekta ya Mifugo imedhamiria kuhimilisha ng’ombe milioni 5 lengo likiwa ni kuhakikisha wafugaji wote nchini wanakuwa na mifugo bora na yenye tija ili kuifanya sekta hiyo kuchangia kikamilifu kwenye pato la taifa.

Pichani ni sehemu ya mitambo iliyopo kwenye Kiwanda cha kutengenezea gesi cha “Tanzania Oxygen Limited (TOL) kilichopo Mkoani Dar-es-salaam ambayo huzalisha  gesi aina ya “Liquid Nitrogen” inayotumika kuhifadhi mbegu kupitia teknolojia ya Uhimilishaji.
Mkurugenzi wa Masoko na Biashara wa Kiwanda cha kutengeneza gesi cha “Tanzania Oxygen Limited” (TOL) Mhandisi Daudi Mlwale (kulia) akielezea hali ya kiwanda chake kuhusu uzalishaji wa gesi aina ya “liquid Nitrogen” kwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Bedan Masuruli (kushoto) na wataalam wa uhimilishaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi walipotembelea kiwanda hicho kilichopo Mkoani Dar-es-Salaam leo (17.08.2021).
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...