Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema
Serikali ipo katika mpango wa kuisimamia biashara ya karafuu ili kuleta
tija kwa serikali na wakulima wa zao hilo.
Ameyasema
hayo leo (Agost 11) wakati alipofanya ziara ya kutembelea mashamba ya
mikarafuu yaliyopo Kichunjuu, Mkoa wa Kusini, pamoja na Mgogoni, Mkoa wa
Kaskazini Pemba, kwa lengo la kusikiliza matatizo yanayowakabili
wakulima wa zao hilo.
Mhe.
Othman amesema kwa muda mrefu zao la karafuu limepoteza uhalisia wake
hasa katika uzalishaji, jambo ambalo kwa kiasi limekuwa likiwarudisha
nyuma wakulima hasa katika kujinyanyua kiuchumi.
"Awali
Zanzibar ilikuwa ikizalisha hadi kufikia kilo elfu ishirini za karafuu
lakini sasa wakulima wamekuwa wakizalisha wastani wa kilo elfu tisa tu.
Mabadiliko haya yanatokana na kukosekana kwa miundombinu bora kwa
wakulima na hivyo kusababisha kupungua kwa idadi ya karafuu inayofika
katika soko la dunia,” alifafanua Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar.
Akigusia juu ya
Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC), Mhe. Othman amesema
bado kumekuwa na tatizo kubwa kwa shirika hilo hasa katika utoaji wa
miche ya mikarafuu, ambayo bado haimnufaishi mkulima katika kuendeleza
ukulima wa zao hilo.
Hata
hivyo, amewahakikishia wakulima kuwa Serikali itaendelea kuwasimamia
katika kuwatatulia matatizo yanayowakabili kupitia mpango unaotaka
kuwekwa, ambao utakuza zaidi biashara ya karafuu na kukuza soko lake
duniani.
Kwa upande wake,
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mhe. Omar Said Shaaban,
amesema katika kuhakikisha uzalishaji wa karafuu unakuwa katika ubora
nchini, Wizara hiyo ina mpango wa kuandaa mkutano na wadau wa karafuu
kwa lengo la kuandaa muelekeo mpya wa kisera na mageuzi katika
uendelezaji wa zao hilo.
"Kutokana
na mabadiliko ya soko la karafuu, serikali inaendelea kupanga bei
ambazo zitakuwa ni mkombozi kwa wakulima pamoja na kuandaa mazingira
rafiki kwa lengo la kukuza uzalishaji wake nchini", alifafanuwa Mhe.
Omar
Naye Waziri wa
Kilimo, Dk. Soud Nahoda Hassan, akizungumzia sifa ya karafuu jambo
ambalo limekuwa tatizo kubwa kwa wakulima, amesema Wizara kwa
kushirikiana na wakulima inaangalia namna ya kuliweka sawa jambo hilo
kwa lengo la kuona tatizo hilo linaondoka na wanafaidika.
Aidha
alisema Serikali ipo katika mpango wa kuwapa mashamba wakulima hao
ambapo kwa sasa Wizara ya Ardhi inaendelea na zoezi la upimaji wa ardhi
kwa ajili ya ugawaji huo.
Nao
wakulima hao wameiomba serikali kuwatatulia matatizo wanayokabiliana
nayo ikiwemo suala la bei ya karafuu, miche pamoja na uharakishaji wa
malipo wakati wanapofanya mauzo yao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...