Na Mwandishi wetu, Simanjiro
Wananchi
27 waliojimilikisha bila uhalali ekari 12,000 ya maeneo ya ardhi ya
Kijiji cha Emboreet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamenyang'anywa
ardhi hiyo na kurejeshwa mikononi mwa Serikali ya Kijiji hicho.
Wananchi
hao 27 walijimilisha ekari 1,000 na wengine ekari 500 tangu mwaka 1993
bila kuwa na nyaraka zozote zinazowaruhusu kumiliki.
Kamishina
msaidizi wa ardhi wa mkoa wa Manyara, Leonard Msafiri ametoa uamuzi huo
wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Emboreet.
Msafiri amesema endapo wananchi hao bado wanahitaji ardhi hiyo wawasilishe maombi na yajadiliwe upya na taratibu zifuatwe.
Amesema
eneo hilo lilitengwa katika mpango wa matumizi ya ardhi ya Emboreet
ambapo matumizi hayakinzani na masuala ya hifadhi ya wanyama pori.
Amesema
ardhi hiyo inabaki kwenye serikali ya kijiji kwa ajili ya matumizi
yaliyoainishwa kwenye mpango wa miaka 10 wa matumizi ya kijiji hicho cha
Emboreet.
"Katika
mgogoro huu unaweza kujiuliza je waliopewa ardhi na wanamiliki kwa
nyaraka gani? je kuna upimaji uliofanyika? je ramani za kipabde cha kila
moja kipo? amehoji Msafiri.
Mkazi
wa kijiji cha Emboreet, Raymond Kosyando amesema wananchi hao
walijimilikisha ardhi hiyo bila kushirikisha wana kijiji ambao ndiyo
wenye mamlaka ya kugawa ardhi.
"Hatuna
shida na wananchi hao ila wanapaswa kutambua kuwa walipata maeneo hayo
bila kuwa na nyaraka zinazowaruhusu kumiliki ardhi hiyo," amesema
Kosyando.
Diwani wa kata
ya Emboreet, Yohana Shinini amempongeza Msafiri kwa kutatua mgogoro huo
wa miaka mingi ambao umezorotesha shughuli za maendeleo za eneo hilo.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa kijiji hicho amewataka wananchi wa eneo hilo
kutoshangilia uamuzi huo kwani hakuna upande ulioshinda na pia wote ni
jamii moja hivyo waendeleze upendo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...