Charles James, Michuzi TV
MADAKTARI Nchini wametakiwa kuwa na huruma kwa wagonjwa ikiwa ni pamoja na kufanya kazi wakizingatia maadili yao na kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa kuwahudumia wagonjwa kwenye maeneo yao.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wakati akifungua mkutano mkuu wa 84 wa mwaka wa Chama cha Madaktari wa Kikristo (TCMA) ambapo amesisitiza watoa huduma hao kufanya kazi kwa weledi na kufuata maadili ya Udaktari.
Askofu Nyaisonga amesema Udaktari ni wito kwani ni kazi ambayo kwa asilimia 100 inahusika na uokozi wa maisha na uhai wa binadamu hivyo kuwasihi Madaktari nchini kuepuka vishawishi vitakavyowafanya waombe na kuchukua rushwa ili kumhudumia mgonjwa.
Amesema ni jambo la kusitisha kuona Daktari ambaye amekula kiapo cha kuwatumikia watanzania kwa maadili na uaminifu akilazimisha kupewa fedha ndio atoe huduma jambo ambalo ni kinyume na maadili ya kazi yao na sheria za Nchi.
" Hivi juzi tumeona video ikisambaa kwenye mitandao mbalimbali ikimuonesha mtoa huduma ya afya kamshona mgonjwa lakini baadaye akakifumua kwa kisingizio kuwa mgonjwa alikua hana hela, bahati nzuri hakua wa Hospitali zetu za Kikristo, kwahiyo kupitia mfano huo niwaombe tuwe na huruma na binadamu wenzetu," Amesema Askofu Nyaisonga.
Amewapongeza Madaktari nchini kwa jinsi walivyoendelea kuwahudumia watanzania katika mazingira magumu ya uwepo wa ugonja wa homa ya Corona (UVIKO-19) pamoja na kukabiliwa na tatizo la rasilimali fedha lakini bado wameendelea kujitoa kuwasaidia wagonjwa.
Ameahidi kwa Serikali kuwa Makanisa ya Kikristo Tanzania yataendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa na kuboresha huduma za afya kwa wananchi kwani Taifa ili liwe imara na kukuza uchumi wake ni lazima liwe na afya bora.
Kwa upande wake Rais wa Chama Cha Madaktari wa Kikristo Tanzania, Dk Bwire Chirangi amesema mkutano huo unajumuisha Madaktari 300 kutoka Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali mbalimbali za Makanisa yote nchini.
Dk Chirangi amesema mashirika na taasisi hizo zinamiliki Zahanati 720, Vituo vya Afya 100 na Hospitali 105 Nchi nzima pamoja na baadhi ya vyuo vya mafunzo ya wauguzi na Madaktari pamoja na vyuo vya kufundishia wataalamu wa ngazi tofauti.
Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA) Dk.Bwire Chirangi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 84 wa mwaka wa maaadaktari hao uliofanyika leo September 6,2021 Jijini Dodoma .
RAIS wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ,Askofu Gervas Nyaisonga,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa 84 wa mwaka wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA) uliofanyika leo September 6,2021 Jijini Dodoma
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...