Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo ameliagiza Jeshi la Polisi hasa Kikosi cha Usalama Barabarani kusimamia sheria za usalama barabarani katika eneo la Mbagala Mzinga ili kunusuru maisha ya wanafunzi wanaosoma katika shule tatu zilizopo maeneo hayo.
Jokate ametoa maagizo hayo mbele ya wananchi wa Mbagala Mzinga baada ya kwenda kukagua maelekezo aliyoyatoa siku za karibuni kutaka yawekwe matuta mawili barabarani kuepusha ajali za wanafunzi zinazosababishwa na madereva wasiozingatia sheria za usalama barabarani ambao wamekuwa wakienda mwendi kasi licha ya kuwepo na idadi kubwa ya wanafunzi na wananchi wanaovuka maeneo hayo.
"Nimekuja kuangalia kama maagizo niliyoyatoa kwa Wakala wa Barabara Tanzania(TANROAD) yamefanyiwa kazi, tayari wameweka matuta na alama za barabarani kama nilivyoagiza, lakini ukiwasikiliza wananchi wa maeneo haya utaona bado kuna madereva wanaendelea kwenda mwendo kasi, hivyo lazima Jeshi la Polisi lichukue hatua zaidi kwa kusimamia sheria za usalama barabarani, madereva waheshimu alama zilizopo.
"Nilazima watu wa usalama barabarani wanyooke kama rula, wafuatilie sana hapa kwa kukamata magari ambayo hayatii sheria za barabarani na zipigwe faini ili nao wajue Serikali ipo , wajue Jeshi la Polisi lipo na wanapopita eneo hili wawe makini kwa kujua wanatembea eneo lenye watoto wengi.Unaweza kuweka matuta na bado wakaenda kasi, hivyo tusipoweza kudhibiti kwa kusimamia sheria bado tutabakia pale pale,"amesema Jokate.
Akifafanua mkakati wa kuondoa changamoto ya wanafunzi kugongwa maeneo hayo, Jokate amesema tayari amezungumza na baadhi ya wadau ambao watakwenda katika shule zilizopo eneo hilo kwa ajili ya kufundisha wanafunzi elimu ya usalama barabarani huku akisisitiza umuhimu wa jeshi la polisi nalo kuendelea kutao elimu ka wananchi namna sahihi ya kutumia barabara kuepuka ajali. Katika eneo hilo kuna Shule ya Msingi Mzinga, Kongowe na Upendo na kwa ujumla kuna wanafunzi zaidi ya 9,000.
Kuhusu msongamano wa magari katika eneo hilo la Mzinga, Jokate aliyekuwa ameambatana na maofisa kutoka TANROAD Mkoa wa Dar es Salaam ba Wilaya ya Temeke wameshauriana namna ya kuangalia uwezekano wa kujengwa kituo cha mabasi kuepusha msongamano uliopo sasa anaotokana na daladala nyingi kusimama barabara kwa ajili ya kushusha na kupakia abiria.
"Mpango wa muda mfupi hapa kuna eneo la shule ya Msingi Mzinga tutajenga kituo cha daladala ili kuondoa hii foleni iliyopo sasa, lakini mpango wa Serikali kwa muda mrefu barabara hii itajengwa njia nne kutokea Mbagala Kuu hadi Kongowe, hivyo hakutakuwa na msongamano tena, niwaombe wananchi , safari yetu ndio imeanza tuwe wavumilivu kwani naamini kwa ushirikiano wetu sisi na ninyi tutafanikiwa, hatushindwa,"amesema.
Kwa upande wa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke Joseph Mwakabonga amesema yote ambayo yameelekezwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke yatatekelezwa."Ni jukumu letu kusimamia maelekezo haya kwa kuhakikisha askari wetu wanakuwepo lakini uwepo wao , tuhahakikisha tunaendelea kusimamia zaidi sheria za barabarani.
Kwa upande wananchi, licha ya kuwekwa kwa matuta hayo, wameendelea kutoa ombi kwa Mkuu wa Wilaya kuwa ni vema yakaongezwa matuta mengine kwa madai kuwa tuta la mwisho kwenye barabara hiyo liko Kipara na kutoka eneo hilo hadi BAKWATA kuna umbali mrefu.
Hivyo madereva wanakwenda mwendo kasi na kufanya dereva hadi akifika eneo la kanisani anakuwa spidi 80 au spidi 90, hivyo zebra ya eneo hilo inakuwa ngumu kuonekana kwa haraka."Kuna mtu anatusaidia kuongoza wanafunzi pale BAKWATA lakini tuta ni muhimu sana."
Kaimu Meneja wa TANROAD Mkoa wa Dar es Salaam Elson Mwelasi amefafanua kwa sasa wameendeelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya barabara na wanajitahidi kuweka alama zaidi kuliko vizuizi labda kuwepo na ulazima sana, hivyo tatizo kubwa liko kwa madereva hivyo ni vema wakatii sheria, na ndio maana katika eneo la Mzinga wameweka matuta mawili kueusha wanafunzi kugongwa.
Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam( wa pili kushoto) akisisitiza jambo alipotembelea eneo la Mzinga kukagua ujenzi wa matuta katika barabara yaliyojengwa kwa lengo la kusaidia kunusuru maisha ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kongowe, Mzinga na Upendo wanaosoma maeneo hayo.Wanaomsikiliza ni viongozi na wananchi
Mkuu wa Wilaya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate(mwegelo) katikati akizungumza wakati alipotembelea eneo la Mzinga kukagua ujenzi wa matuta ya barabarani kuepuka ajali zinazotokea kwa wanafunzi wanaogonjwa wakati wanavuka barabara.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo akiwasilimia wanafunzi wa darasa la Saba wa Shule ya Msingi Mzinga baada ya kutembelea shuleni hapo, akiwa hapo Jokate amewakumbusha wanafunzi kuwa makini wakati wakivuka barabara
Kaimu Meneja wa Tanroad Elson Mwelasi( wa pili kushoto) alitoa ufafanuzi kwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo baada ya kutembelea eneo hilo kukagua maelekezo aliyoyatoa kuhusu kujengwa matuta na alama za usalama barabarani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...