Na Amiri Kilagalila,Njombe
Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe kimewaonya
wanaotaka kuteuliwa na chama hicho kugombea udiwani kata ya Luduga
kutoshiriki vitendo vya rushwa vinginevyo watachukuliwa hatua za
kinidhamu.
Onyo hilo
limetolewa leo na katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilayani humo Juma
Nambaila wakati akitaja wagombea waliopitishwa na chama hicho kugombea
nafasi ya udiwani kata ya Luduga.
Amesema
wagombea nane wa chama hicho ambao wamepitishwa ngazi ya wilaya
kugombea wanatakiwa kufuata miiko na taratibu za uchaguzi wa Chama cha
Mapinduzi ili apatikane atakayeshinda kihalali.
Amesema
endapo wakikiuka kanuni zilizowekwa kwa kutoa rushwa ili majina yao
yapitishewe na chama hicho kugombea udiwani kata ya Luduga watachukuliwa
hatua za kinidhamu.
Amesema
wilaya ya Wanging'ombe ni miongoni mwa kata sita mkoani Njombe ambazo
zimetangaziwa kufanya uchaguzi mdogo na mkurugenzi wa tume ya taifa ya
uchaguzi ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo za kifo.
Amesema
kata ya Luduga iliyopo wilayani humo inalazimika kuingia katika
uchaguzi mdogo baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo Hassan Ngella
kufariki dunia miezi miwili iliyopita.
Amesema
chama hicho ngazi ya wilaya baada ya kupokea maagizo kutoka
kiliwatangazia wanachama kata ya Luduga ili kujitokeza kuwania nafasi
hiyo ambayo kwasasa ipo wazi.
Amesema
wagombea walichukua fomu na kurudisha kati ya tarehe 5 na 6 mwezi huu
ambapo wanachama tisa walijitokeza kuchukua fomu ya kugombea udiwani na
nane pekee walifanikiwa kurudisha fomu hizo na kukidhi vigezo.
"Tarehe
saba mwezi huu tulikuwwa na mkutano maalum wa kura za maoni katika kata
ya Luduga ili kuwapigia kura miongoni mwa hao waliorudisha fomu hizo"
amesema Nambaila.
Amesema
uchaguzi wa awali umefanyika kwa lengo la kumpata atakayeongoza katika
kura za maoni ili vikao vingine vyenye mamlaka ya kutoa maoni na kuteua
viweze kukaa na kumpitisha mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya
chama hicho.
Mwenyekiti
wa Chama cha Mapinduzi wilayani humo Stephano Kinyangazi amesema kazi ya
kamati ya siasa ya wilaya hiyo ni kupitia majina na sifa za wagombea
kisha kuyapeleka kamati ya siasa mkoa jambo ambalo tayari
limeshafanyika.
Amesema
anaamini kamati hiyo ngazi ya mkoa itatekeleza majukumu yake vizuri
pasipo shaka kwani wana uzoefu kwakuwa siyo mara yao ya kwanza.
"Tunategemea
atakayechaguliwa tutashirikiana pamoja kuhakikisha nafasi hiyo
anachukua endapo kitajitokeza chama cha upinzani" amesema Kinyangazi.
Mmoja
ya wagombea waliojitokeza kuwania kuteuliwa kuwa mgombea udiwani kata
ya Luduga Belshaza Mhanga amesema iwapo chama chake kitampitisha
kugombea nafasi hiyo na kushinda kwenye uchaguzi ataanza na ujenzi wa
kituo cha afya kwa kushirikiana na wananchi na serikali.
"Kama
nitashinda moja kati ya mambo nitakayoanza nayo ni kusimamia ujenzi wa
kituo cha afya kwa kushirikiana na wananchi na serikali" amesema Mhanga.
Miongoni
mwa wagombea waliopitishwa na chama hicho kuwania kuteuliwa kugombea
udiwani kata ya Luduga ni pamoja na Belshaza Mhanga, Andrea Maseleka,
Yaledi Mlyuka, Jacob Kilinyi, William Kinywafu, Jaston Chengula, Setti
Munganile na Ayoub Fute.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...