Na Joseph Lyimo, Simanjiro
LIKIZO
isiyo ya lazima kwa wanafunzi wa shule za msingi kwenye Wilaya ya
Simanjiro Mkoani Manyara, kwa sababu ya ugonjwa COVID 19 ilisababisha
wasichana 50 wasiendelee na masomo yao kutokana na kufungwa shule kwa
takribani miezi mitatu mwaka jana.
Inaelezwa
kuwa wanafunzi hao walishindwa kurudi masomoni kutokana na kuolewa au
kupata ujauzito kutokana na baadhi ya wazee wa jamii ya kifugaji kutumia
fursa hiyo ya likizo na kuwaoza mabinti hao.
Wanafunzi
50 wa shule ya msingi Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, waliacha shule
kwa kuolewa wakiwa wadogo au kupata ujauzito kutokana na kuwa majumbani
mwao kipindi cha likizo ya takribani miezi mitatu ya Covid 19.
Ofisa
elimu wa shule za msingi Wilaya ya Simanjiro, Silvanus Tairo amesema
likizo hiyo iliyotokana na Covid 19 ilisababisha wanafunzi hao kuacha
masomo yao na hawakurudi shuleni baada ya shule kufunguliwa.
Tairo
amesema shule zilifungwa kutokana na Covid 19 Machi 17 mwaka 2020 na
kufunguliwa Juni 29 mwaka 2020 na wakabaini baadhi ya wanafunzi
hawakurudi masomoni.
Mmoja
kati ya viongozi wa kimila wa (Laigwanani) Yohana Ole Tiamongoi
amesema, viongozi wa kimila wa eneo hilo wamekuwa wakikubaliana kwenye
vikao vyao kila mara kuwa suala la watoto wa jamii ya kifugaji kupatiwa
elimu liwe ni kipaumbele.
“Jamii
yetu imekuwa na mwamko wa kuwapatia elimu watoto wote wakifugaji
wakiume na wakike japokuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya wenzetu
wanamtazamo hasi kwa mtoto wa kike kuwa bado ni wakuolewa na siyo kupata
elimu,” amesema Ole Tiamongoi.
Mchungaji
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Arusha
Mashariki, Usharika wa Purana, Enock Paulo amesema hivi sasa jamii ya
kifugaji imebadilika kwa kuhakikisha watoto wao wanapata elimu.
Mchungaji
Paulo amesema jamii ya kifugaji inawasomesha watoto wakiume na watoto
wakike wasidhani ni wakuolewa pekee kama walivyokuwa wana dhana potofu
miaka iliyopita.
Amesema
watoto wa kike wana msaada mkubwa kwa jamii ya kifugaji na anapaswa
kuolewa akifikisha umri wa miaka 18 kwa asilimia kubwa wengi
wameelimika kwenye suala la kusomesha watoto wao.
“Jamii
ina kazi kubwa kuwapeleka shule watoto wao hasa wa kike kwani wanakuwa
na uwezo mkubwa wa kusababisha mabadiliko kwenye familia na hata taifa
kwa ujumla,” amesema mchungaji Paulo.
Amesema
hivi sasa jamii ya kifugaji imekuwa na mwamko mkubwa wa kusomesha
watoto wao ili kuhakikisha wanakuwa na chachu ya maendeleo kwa miaka
inayokuja.
Mwenyekiti wa
kijiji cha Naisinyai, Merika Makeseni anasema kwenye kijiji chake
hakukuwa na mwanafunzi hata mmoja ambaye aliacha masomo kipindi cha
likizo ya Covid 19 mwaka jana kwani wazazi na walezi, walishaelezwa kuwa
wanafunzi wanapaswa kupatiwa elimu na siyo kuozeshwa wakiwa wadogo.
"Kwa
kweli jamii ya kifugaji ya kimasai kwa upande wa Naisinyai imebadilika
kwenye mtazamo wa kusomesha watoto hasa wakike kwani tunaona faida kubwa
ya elimu hivi sasa" amesema Makeseni.
Mkuu
wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt Suleiman Serera, hivi karibuni alikutana na
wakuu wa idara ya elimu na kuwaagiza kuandaa na kuweka mpango mkakati
wa kupunguza na kukabiliana na tatizo la utoro na mimba za utotoni kwa
wanafunzi katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.
Dkt
Serera amesema baadhi ya wanafunzi wa kike wamekuwa wakikatisha masomo
yao kutokana na kupata ujauzito na wengi kushindwa kuhudhuria masomo
baada ya kubebeshwa mimba bado wakiwa wanasoma.
"Wakuu
wa idara za elimu mnapaswa kuweka mpango mkakati ambao utatekelezeka
ili kupunguza na kuondoa kabisa tatizo la utoro na mimba kwa wanafunzi
wa shule za msingi na sekondari," amesema Dkt Serera.
Ametoa
rai kwa wataalamu hao wa idara ya elimu, kuwashirikisha wazawa
waliopata fursa ya kupata elimu, kushawishi wazazi na walezi wa eneo
hilo, kuwapeleka watoto wao shule.
Pia,
amewaagiza wahahakikishe wanafunzi wanahudhuria masomo kwa vipindi
vyote vya muhula wa masomo na kuimarisha mfumo wa elimu kwa watu wazima
(MEMKWA).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...