Na.Vero Ignatus,Arusha.
Imeelezwa kuwa Kufuatia utafiti wa uboreshaji wa zao la migomba aina ya Mshare Kanda ya Kaskazini ,uliofanyika takribani miaka nne kuanzia mwaka 2015-2016; uliofanywa na wataalamu wa tafiti kutoka ndani na nje ya nchi, umekuwa na mafanikio makubwa kwa zao hilo hapa nchini Tanzania.
Hayo yameelezwa na Mtafiti Mwandamizi kwenye zao la ndizi ,ambaye pia ni Meneja wa Taasisi ya Utafiti Tanzania TARI-TENGERU Dkt. Mpoki Shimwela alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, kuhusu mradi wa majaribio wa kupata mbegu bora za ndizi Mshare ,ambao unatekelezwa kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la Utafiti wa Kilimo Ukanda wa Kitropiki (IITA),mradi wa shamba la majaribio lililopo eneo la Chuo Kikuu cha Nelson Mandela mkoani Arusha.
Aidha ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza nchi ya Tanzania, kupitia watafiti wa kilimo wamefanikiwa kuzalisha mbegu za migomba ya ndizi aina ya Mshare, na kwamba hatua iliyofikiwa sasa bado kuna hatua nne za utafiti wa zao wa migomba, ambapo itachukua takribani mwaka mmoja na miezi sita hadi kuvunwa, ambapo kwa wastani wa kipindi cha miaka mitatu hadi minne ,ili kuweza kuwapelekea wakulima wa zao hilo.
Dokta Mpoki ameongeza kuwa licha ya jitihada ambazo zinafanywa na watafiti hao lakini kumekuwa na changamoto kadhaa ikiwemo zao hilo la migomba kutokuwa na mbegu,ambapo hali hiyo inawawia vigumu watafiti kupata mbegu za kutosha kufikia malengo yao.
Naye Meneja Mradi huo Dkt SWENNEN RONY kutoka Shirika la Utafiti wa Kilimo Ukanda wa Kitropiki (IITA); amesema wameshirikiana na Taasisi ya Utafiti Tanzania TARI-TENGERU kufanya utafiti huo kwani Ndizi Mshare na Matoke ni chakula cha asili Tanzania na Uganda, lengo likiwa ni kuboresha mpango wa kitaifa na kimataifa katika utafiti wa zao la migomba sambamba na kuwajengea uwezo watafiti wa Kilimo nchini Tanzania ili kupata mbegu bora zaidi kati ya zile wanazoendelea kutafiti; kabla ya kuwafikia wakulima.
Kwa upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya Uthibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) Kanda ya Kaskazini Mungu Atosha Ngomuo amesema lengo la uwepo wa TOSCI katika mradi huo wa majaribio ya kuzalisha mbegu za migomba na kufuatilia hatua za mbegu hizo zenye ukinzani na ugonjwa wa mnyauko (Fusaria) wa migomba na kupitia hatua za utambuzi wa mbegu zilizozalishwa na watafiti sambamba na kuhakikisha mbegu zinazowafikia wakulima ziko katika ubora uliokusudiwa kulingana na sheria zilizopo.
Kwa upande wao Elishi Karisa Kitomari ambaye ni mkulima wa zao la ndizi aina ya Mshare na Evelini Kiliomana ambaye ni mfanyabiashara wamewaomba Watafiti wa mazao ya kilimo kuendeleza jitihada za kupata suluhisho la ugonjwa wa mnyauko ambao umekumba zao hilo, ambalo lipo hatarini kutoweka na kuathiri kipato cha mkulima jambo ambalo linawapa hofu.
Wakulima hao wamesema kuwa endapo watafiti hao watakuja na suluhisho la kudumu kufuatia utafiti wa zao hilo la ndizi Mshare itawasaidia kurejesha matumaini mapya ya kupata chakula cha uhakika na kukuza kipato chao kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.
Mradi huo wa Utafiti wa uboreshaji wa mbegu bora za migomba umegawanyika katika maeneo manne ikiwemo uboreshaji wa zao la migomba ya ndizi Bukoba au Matoke utafiti wake umeanzia nchini Uganda na kuendelea hapa nchini Tanzania, utafiti wa Uboreshaji wa migomba aina ya ndizi jamii ya mshare unaofanyika nchini Tanzania, kwa kuendeshwa na TARI Tengeru, Uyole, Ifakara na Maluku kwa majaribio katika vituo hivyo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...