David Francis Matongo

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

VIJANA ambao walipata ufadhili wa kusomeshwa Chuo cha urembo cha Maznat jijini Dar es Salaam wametoa shukrani zao kwa Shirika la Childbirth Survival International(CSI) ambalo liliamua kubeba jukumu la kuwagharamia masomo yao, kwani hivi sasa wanaendesha maisha yao kupitia ujuzi walioupata katika chuo hicho.

CSI kupitia programu maalum yake ya kuwasaidia vijana kutimiza ndoto zao Januari mwaka huu waliandaa zoezi la kutafuta vijana wawili kwa ajili ya kuwafadhili kusoma kwenye chuo hicho ambapo kati ya vijana zaidi ya 100 waliojitokeza wawili walipata ufadhili.

Kwa mujibu wa CSI, wameamua kuungana na vijana katika  kuwasaidia wakiamini vijana ndio wazazi wa kesho, na akiwezeshwa kiuchumi itakuwa rahisi kumudu kuhudumia familia yake, hivyo kupunguza changamoto za kimaisha zikiwemo za kumudu gharama za matibabu ya afya hasa katika kupunguza vifo kwa mama mjawazito na mtoto.

Akizingumza leo Septemba 8, 2021 katika mahojiano maalum David Francis Matongo ambaye ni mmoja ya wanufaika wa mradi wa kusaidia vijana wa kutimiza ndoto zao kupitia ufadhili huo amesema tangu alipomaliza masomo ya urembo na upambaji maisha yake yamekuwa na tofauti kubwa kwa sasa anajimudu kimaisha.

"Mwanzoni sikuwa nalijua Shirika la CSI lakini kupitia shughuli wanazozifanya hasa za kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, kuna ndugu zangu walinifuata na kuniambia kuhusu shirika hili na wakati huo walikuwa wakitafuta vijana wa kuwasaidia ili kuwasomesha, hivyo walinishauri nikajaribu bahati yangu na kweli ikafanikiwa kuipata.

"Nakumbuka ilikuwa Januari mwaka huu ndio waliitisha zoezi kutafuta vijana, tulikuwa wengi na mimi na mwenzangu mwingine ambaye hivi sasa anaishi  Dodoma tulichaguliwa na Februari 19, 2021 tukaanza masomo Maznat, CSI iligharamia kila kitu kuanzia ada, fedha ya usafiri na kugharamia vifaa vyote vilivyohitajika.

"Tukiwa Maznat tulijifunza mambo yanayohusu  urembo pamoja na upambaji. Ukweli CSI imenisaidia kujikwamua na umasikini kwa namna fulani, kupitia ufadhili wao wa  masomo naweza kujikimu kimaisha.

"Kwa sasa naweza kuamua kuajiri au kuajiriwa na shirika lolote kwani kazi ninayofanya nimesomea na walifanikisha masomo yangu ni CSI. Baada ya kumaliza chuo nimekuwa nikiwahudumia watu mbalimbali ambao wanakuja kwa ajili ya kufanya urembo aidha wa kucha, kusuka au kupaka rangi,"amesema na kusisitiza kupitia kazi hiyo anapata fedha za kujikimu kimaisha.

Amefafanua akiwa Maznat wamesoma mambo mengi yanayohusu urembo na upambaji yakiwemo kupamba bibi harusi, kupamba majukwaa, kutengeneza mtu kucha, kufanya masaji , kusuka na kufanyia mtu make Up.

Matongo ameweka wazi kabla ya ufadhili wa CSI aliamiani kazi ya urembo na kupamba ni ya wanawake tu lakini amebaini kazi hiyo inafanywa hata na mtu yoyote bila kujali jinsi na kwake anajisikia fahari kubwa.

Amefafanua ameamua kujikita katika kutengeneza kucha, kusuka na Make Up."Kuna tofauti kubwa kabla ya kwenda chuoni na sasa, zamani nilikuwa nakaa nyumbani na siwezi kuingia fedha lakini leo hii nakaa nyumbani na watu wanakuja nawahudumia, tayari ninao ujuzi unaoniingizia kipato, na ninawashukuru sana CSI kwa ufadhili wa masomo."

Pamoja na shukrani hizo ametoa ombi kwa CSI kuwa anatamani kuona wakiendelea kumshika mkono na hasa kumsadia kupata vifaa na eneo maalum za kufanya kazi zake."Nikiwa na vifaa na eneo langu maalum la kufanya kazi nitaongeza wigo wa kipato changu."

Aidha amesema malengo ya CSI kuandaa vijana kuwa baba bora na mama bora kwa siku za baadae anaona yanavyofanikiwa kwani yeye binafsi ameanza kupata fedha kupitia kazi anayofanya, hivyo inampa uhakika wa kumudu kuhudumia familia.

"Nawashukuru CSI kuniwezesha kutimiza ndoto zangu, niombe waendelee kusaidia vijana wengine kwani wako wengi mtaani na wanatamani  kupata fursa ya kusoma kama mimi lakini kutokana na kipato duni wanashindwa, hivyo ni wakati wa CSI kuendelea kuwasaidia vijana, tunatambua mchango wao katika kuunguza vifo vya mama wajawazito na watoto lakini waendelee kutusaidia vijana,"amesema

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...