Raisa Said,Bumbuli.


SERIKALI imetoa jumla ya Sh  million 306.7 kwa ajili ya ukarabati wa barabara zilizomo katika Halmshauri ya Wilaya ya Bumbuli, Mkoani Tanga  ili kutatua changamoto ya barabara inayoikabili Halmashauri hiyo.

Akizungumza wakati akikabidhi Mkataba kwa Wakandarasi waliopewa kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 59.7, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kalist Lazaro alisema ukarabati huo utahusu matengenezo ya maeneo korofi na matengenezo maalum

 Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa Serikali ya Awamu ya sita imedhamiria kutatua changamoto za  vijijini ikiwemo ile ya barabara.

Lazaro alisema kuwa Mkataba huo alioukabidhi  unatakiwa utekelezwe ndani ya miezi sita hivyo alimtaka Mkandarasi  huyo wa Kampuni ya Simjo Tech Company kutoka mkoani Kilimanjaro afanye kazi  kwa mujibu wa Mkataba.

“Tunataka na kazi bora na thamani ya fedha ionekane hivyo lazima uhakikishe kazi hiyo inakamilika kwa wakati,” alimwambia mknadarasi huyo.Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza kuwa hatawavumilia wakandarasi watakaoshindwa kutekeleza miradi kwa wakati katika Wilaya ya  Lushoto.

"Rais wetu ametupatia fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara zetu ili zipitike muda wote hasa wakati wa mvua hivyo. Wakandarasi watakao shindwa kumaliza kwa wakati sitawavumlia,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Meneja wa Wakala wa barabara (Tarura), Bumbuli,  Theophilda Domician, alisema kuwa awali bajeti yao ilikuwa ni Sh milioni 686.96 kwa ajili ya barabara zote za Bumbuli. Alieleza kwamba, hata hivyo, kwa hisani ya Rais Samia akaongeza sh billion 1 kwa ajili ya barabara ambazo mikataba yake inaandaliwa na iko katika hatua ya manunuzi  pamoja na sh.million 500 kwa ajili ya barabara ya lami  Bumbuli.

Alitaja barabara ambazo zitajengwa kwa kiwango cha changarawe kuwa ni pamoja na barabara ya Baga Mgwashi - Mbelei (23.8 km), Bumbuli -Mayo, Vulii- Mahezangulu hadi (15.4 km), barabara ya Vuga - Mponde hadi Wena yenye urefu wa (kilomita 21.2) na barabara ya Balangai - Tamota hadi Vulii (km 13).

 Meneja huyo pia alieleza kwamba wamepatiwa sh billion 3.5 kwa ajili ya barabara ya Mlalo- Mlola hadi Millingano na kwa Bumbuli kuna kilometa 26 ambazo tayari ziko katika hatua za manunuzi.

 Alizitaja barabara zitakazojengwa na Mkandarasi huyo wa Simjo na ambazo zitakazofanyiwa matengenezo maalum kuwa ni barabara  ya Milingano-Yamba, Mbelei-baga-Mgwashi, barabara ya Mashewa-Milingano -Mlola na barabara ya Milingano -Kwediwa pamoja na barabara ya Mbelei-Baga-Mgwashi ambayo itafanyiwa matengenezo kwenye sehemu korofi.

 Kuhusu ujenzi wa vivuko kwenye barabara ya Mgwashi Malomboi na Mbelei-Baga hadi Mgwashi,kwa upande wake, Mkandarasi aliyesaini Mkataba wa miradi hiyo,  John Kavuta, alisema licha kupewa miezi sita ya kutekeleza miradi hiyo wao watatekeleza kwa miezi miwili tu.

Kavuta alisema anachoomba kwa wananchi wawape ushirikiano sababu yeye sio mgeni wa kufanya kazi katika Halmashauri ya Bumbuli .

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halamshauri  hiyo, Hozza Mandia, alisema endapo barabara hizo zitakamilika zitawasaidia wananchi na wakulima kupitisha mazao yao kwa muda wote.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...