WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema vyombo vya ulinzi na usalama nchini vimeendelea kufanya kazi ya kudhibiti matukio mbalimbali ya vitendo vya kihalifu ukiwemo wizi wa mifugo.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 9, 2021) wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo alitaka kujua Serikali imejipangaje katika kudhibiti na kukomesha matukio ya wizi wa mifugo yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu amesema mbali na hatua zinazochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama pia, Serikali inawashirikisha wananchi katika ulinzi shirikishi ili kudhibiti vitendo hivyo.

“Tumedhibiti sana usafirishaji holela wa mifugo ikiwemo ng’ombe kutoka eneo moja kwenda lingine. Ng’ombe sasa hawezi kusafirishwa kwenda lingine bila ya kuwa na kibali maalumu.”

Amesema Serikali imeendelea kuwaelimisha wafugaji kufuga kulingana na ukubwa wa maeneo yao pamoja na kujenga mabanda imara ya kufugia mifugo yao.

Pia, Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na wizi wa mifugo Serikali imeanzisha mfumo wa utambuzi wa ng’ombe kwa kutumia hereni za kielektroniki ambao unaonesha mliki wa mfugo na eneo, hivyo kurahisisha utambuzi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi hususan waendeshaji wa vyombo vya moto wafuate sheria zilizowekwa bila ya kushurutishwa yakiwemo matumizi sahihi ya barabara badala ya kuliachia Jeshi la Polisi pekee.

“Tunatarajia kila Mtanzania atatimiza wajibu wake bila ya kushurutishwa na matumizi ya barabara yameanishwa kikamilifu kupitia sheria zetu na usimamizi unaendelea kwa vyombo ambavyo tumevipa jukumu hilo.”

Waziri Mkuu amesema kuwa licha ya Jeshi la Polisi kuwaelimisha Watanzania matumizi sahihi ya barabara kupitia vyombo mbalimbali vya habari lakini bado kuna baadhi ya watumiaji wameendelea kukiuka sheria.

“…Ni muhimu kwa watumiaji wote wa vyombo vya moto kuzingataia sheria za barabarani kwa sababu inalinda uhai wa Watanzania.”

Waziri Mkuu ameyasema wakati akijibu swali la mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba aliyetaka kujua kauli ya Serikali katika kuhakikisha watumiaji wa vyombo vya moto wanafuata sharia za usalama barabarani.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu swali Bungeni jijini Dodoma



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisikiliza swali kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko (kushoto) , Bungeni jijini Dodoma, Septemba 9, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



Mbunge wa Mlalo, Rashidi Shangazi akimuuliza swali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Bungeni jiini Dodoma, Septemba 9, 2021. Kushoto ni Mbunge wa Viti Maalum, Mwantumu Zodo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...