NA MWANDISHI WETU.
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ni miongoni mwa Taasisi za mwanzo kujiunga na Mfumo wa Utoaji Huduma wa Pamoja wa Serikali (One Stop Service Centre) ambao Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameuzindua leo Septemba 6, 2021 jijini Dar es Salaam.
WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, amezitaka Taasisi nyingine za Serikali ambazo bado hazijajiunga na Mfumo huo unaoratibiwa na Shirika la Posta Nchini, kuhakikisha zinajiunga ndani ya mwaka huu wa fedha wa 2021/2022.
“Mradi huu unaenda kubadilisha namna ya utoaji huduma bora, ni muhimu kuharakisha na kuhakikisha kwamba unafanikiwa, hivyo basi nazielekeza taasisi zote zinazotoa huduma kuongeza kasi ya kujiunga na Utaratibu wa Utoaji Huduma wa Pamoja.” Alisisitiza.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndungulile amezitaja Taasisi ambazo tayari zimeanza kutoa huduma kupitia mfumo huo kuwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Vizazi na Vifo (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Idara ya Uhamiaji, BRELA, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NHIF) na benki ya CRDB.
Kwa kuanzia Mfumo huo tayari umezinduliwa kwenye mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam na kwamba lengo ni kufikia mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani, alifafanua Dkt. Ndungulile.
Akizungumza pembezoni mwa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), C.P.A Hosea Kashimba alisema, Taasisi yake iliamua kujiunga mara moja na Mfumo huo kwa sababu Mfuko unawajali Wanachama na Wateja wake.
“Tumeona utaratibu huu ni mzuri, utapelekea kumuhudumia mwanachama kwa haraka lakini pia kuondoa usumbufu ambao pengine mwanachama anaweza kukutana nao hivyo anaweza akafika hapa na kuhudumiwa na kama kuna taarifa zinahitajika kutoka Taasisi nyingine Taasisi hizo nyingine ziko hapa ikiwemo NIDA, RITA na Taasisi ambazo tunashirikiana katika kutoa huduma.” Alifafanua C.P.A Kashimba.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...