Na Woinde Shizza , ARUSHA
SHIRIKA la umeme Tanesco mkoa wa Arusha linakabiliwa na tatizo la kuibuka kwa wimbi kubwa la vishoka pamoja na wateja kulaghaiwa na kujengewa miundombinu ya umeme na kuchezea mita kinyume na taratibu.
Kutokana na hali hiyo shirika hilo limeanzisha ukaguzi maalum wa kukagua meter kwa ujumla na takribani wateja 7,432 wamekaguliwa Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita kwa ajili ya kuwakamata waliohusika na matatizo ya kuchezea mita pamoja na vishoka waliowafanyika kazi hizo.
Hayo yamebainika na meneja wa Tanesco mkoa wa Arusha mhandisi Herini Mhina wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alisema kuwa katika ukaguzi huo jumla ya wateja 97 wamekamatwa na matatizo mbalimbali yakiwemo ya kuchezea mita na wanatarajia kukusanya kiasi cha shilingi 130,315,215.41 kama faini ya uchezeaji mita ambapo alifafanua kuwa kati ya hizo teari wamefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 14,719,096.40.
Alisema kuwa pia Katika zoezi hilo wateja 29 waling'olewa nguzo za miundombinu ya umeme kutokana na kuunganishiwa umeme kinyume na taratibu na takribani kiasi cha shilingi 31,603,360.88 kinatarajiwa kukusanywa kama faini na kesi dhidi ya matukio hayo ziko mahakamani zikingojea hatua za kisheria kufuatwa.
Mhina alifafanua kuwa kutokana na tatizo matatizo hayo wao kama shirika la umeme Tanesco tatizo lingine linalowakabili ni pamoja na baadhi ya wananchi kuhujumu miundombinu yao kwa kuchoma mashamba kipindi wanapotayarisha mashamba kwa ajili ya msimu wa kilimo.
Alitoa wito kwa wananchi wote wamkoa wa Arusha na maeneo mengine kuepuka kutumia mafundi ambao hawajaidhinishwa na mthibiti wa EWURA,kukagua miundombinu ya utandazaji umeme majumbani mwao kola baada ya miaka mitano, kufuata taratibu za upatikanaji wa umeme kupitia ofisi zao zilizopo karibu nao.
Aliongeza kuwa malipo yoyote ya utandazaji nyaya za umeme majumbani ni makubaliano ya mteja na fundi ,au kampuni kufanya kazi kuchora mchoro na kugonga muhuri pamoja na kutoa risiti ya EFD na wananchi wanapaswa kujua malipo yote ya serikali yanafanywa kupitia Control number hivyo ni bora wakawa makini ili wasitapelewe huku akibainisha kuwa ni marufuku kutoa rushwa au hela kwa mfanyakazi yeyote wa Tanesco.
Mhina alisema kuwa wao kama shirika wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari kuwa ni jukumu lao kusaidia kulinda miundo mbinu inayowekwa na itakayowekwa kwenye maeneo yao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...