Uingereza imeipongeza Tanzania kwa hatua za kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji, Haki za Binadamu na Utawala Bora, jambo ambalo limeimarisha ushirikiano baina ya Nchi hizo. 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameyasema hayo wakati wa mazungumzo kwa njia ya mtandao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge, ukiwa ni utekelezaji wa mazungumzo ya awali kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri huyo alipofanya ziara hapa nchini.

 

Balozi Mulamula ameongeza kuwa kutokana na mazungumzo hayo Uingereza na Tanzania zimekubaliana kufanya kongamano kubwa litakalojumuisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uingereza ili kuja kuwekeza hapa nchini. 

 

Pia Balozi Mulamula ameishukuru Uingereza kwa kuiunga mkono Tanzania katika bodi ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) jambo lililoiwezesha Tanzania kupata mkopo wa masharti nafuu wa shilingi Trilioni 1.3 kwa ajili ya kukabiliana na adhari za UVIKO 19.

 

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami, ambapo ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kulisaidia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ili kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo kuwarejesha wakimbizi makwao kwa hiari.

 

 “Ili shirika hili liendelee kuhudumia vyema wakimbizi ni muhimu Jumuiya ya Kimataifa ikaendelea kutoa mchango wake, hasa kwa kuwaongezea bajeti UNHCR ambayo itawawezesha kutimiza majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi zaidi” alisema Mheshimiwa Balozi Mulamula 

 

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami kwa niaba ya Shirika hilo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania kwa kuendelea kutoa mchango wa muda mrefu katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi. 

 

Ofisi ya Kikanda ya UNHCR iliyopo Kasulu, Kigoma inahudumia nchi Kumi na Moja (11) ambazo ni; Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, South Sudan, Tanzania and Uganda.

 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika mazungmzo na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dodoma Septemba 09,2021

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...