Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imeendelea kuwafikia wananchi wa maeneo ya pembezoni mwa mji baada ya miradi mbalimbali kutekelezwa.
Maeneo hayo ni yale yaliyopo nje ya mtandao rasmi wa maji katika miji ya pembezoni ambapo Mojawapo ya miradi inayotekelezwa ni Mradi wa Minondo uliopo katika mtaa wa Minondo kata ya Somangila Halmashauri ya Kigamboni.
Mradi huo una takribani miaka 48 toka kuanzishwa kwake mwaka 1973 kabla ya uanzishaji wa serikali za vijiji mwaka 1974-75 kwa lengo la kuhamisha watu waliokuwa wakiishi pembezoni mwa bahari ili kutunza mazingira ya bahari.
Mradi wa Minondo ulikuwa unahudumia kaya 20 tu na ongezeko la watu, uchakavu wa miundombinu na usamamizi mbovu wa mradi ilipelekea mradi huu kutokufanya kazi kwa ufanisi.
Kutokana na changamoto hizo DAWASA iliamua kuufufua mradi huo na kufanyia maboresho mwaka 2020 ili kuboresha huduma ya majisafi na kuongeza mitandao ya majisafi ili kukidhi mahitaji ya huduma hii.
Mamlaka imefanya maboresho katika mambo mbalimbali katika chanzo cha maji (kisima cha Minondo) kwa kupima wingi wa maji, kusafisha kisima, kufanya maboresho katika chanzo cha maji kwa kupaka rangi.
Maboresho mingine yaliyoweza kufanyika ni kuziba maeneo yaliyokuwa yanavuja katika tenki la kuhifadhi maji, kusafisha eneo la tenki,kulaza bomba la inch 2 kwa umbali wa kilomita 1.1 kutoka kwenye chanzo hadi kwenye tenki na kuongeza mtandao wa majisafi kwa umbali wa kilomita 1.8 .
Kutokana na maboresho haya yanayofanywa na DAWASA kwa sasa mradi una uwezo wa kuhudumia kaya zaidi ya 1000 na wananchi zaidi ya 4,218.
Wateja takribani 121 wameshaunganishiwa huduma ya maji na DAWASA pia imejenga vituo vitatu vya kuchotea maji (vioski) ambavyo vinahudumia wananchi wale ambao bado hawajaweza kujiunganishia maji majumbani .
Akizungumzia mradi huu wa Minondo – Kigamboni, Mtendaji wa Mtaa wa Minondo Bi Riziki Chaurembo ameipongeza DAWASA kwa kuweza kuboresha mradi wa maji Minondo ambao kwa sasa wananchi wameanza kunufaika kwa kupata huduma ya majisafi kwa umbali mfupi na gharama nafuu.
“Naishukuru DAWASA kwa kufanikisha uboreshaji wa mradi huu wa maji ambapo kwa sasa unawasaidia wananchi katika eneo hili ili kwa huduma ya majisafi…” alisema Bi Chaurembo
Aliongezea kuwa Mamlaka izidi kulaza mabomba ili wananchi wengi wafikiwe , hasa wananchi wa maeneo ya Shinyanga, Mwembe na Gomvu – Center.
“Ninaiomba DAWASA iendelee na matengenezo katika ulazaji wa mabomba ya maji ili yasaidie kuwahudumia wananchi waishio katika maeneo tofauti tofauti kama vile Shinyanga, Mwembe na Gomvu – Center..” alisisitiza Bi Chaurembo.
Hata hivyo, Mradi huu wa Minondo – Kigamboni kupitia chanzo cha maji (kisima cha Minondo) kina uwezo wa kuzalisha maji lita 15000 kwa saa na tenki la kuhifadhia maji lina uwezo wa kutunza maji lita 45000 kwa saa.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...