Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
WATAALAM wa masuala ya Vinasaba vya binadamu Tanzania wameungana na wataalamu wenzao wa vinasaba vya binadamu Bara la Afrika kwa ajili ya kujadiliana mambo mbalimbali ya vinasaba katika kuboresha afya za waafrika na dunia kwa ujumla.
Akizungumza wakati akifungua Kongamano hilo linaloendelea jijini Dar es Salaam , Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Mhe Nassor Mazrui amesema kongamano hilo ni muhimu katika sekta ya afya hasa kwa kutambua umuhimu wa vinasaba vya binadamu..
Amesema kupitia watalaamu hao wa vinasaba vya binadamu wakiweka mikakati na kufanya tafiti za vinasaba itasaidia pia kukabiliana na magonjwa yanayosumbua dunia ukiwemo ugonjwa wa Covid- 19.
" Kama mnavyojua sisi sasa hivi kwa miaka miwili tunasumbuka sana na Uviko ,imekuwa changamoto ya dunia nzima mpaka sasa tumeanza chanjo na watu wengi sana wamo katika mshangao lakini kwa kweli sisi kama Tanzania au Afrika tunaweza kuwa na mchango mkubwa zaidi kuliko huko Ulaya katika suala la Uviko 19 linalotutaza.
" Hawa mabingwa wetu katika vinasaba vya binadamu wakipewa fursa kubwa zaidi kufanya utafiti wanaweza kuja na kitu kizuri,hivyo nasema Tanzania ipo haja ya kuanzisha data ambayo itaonesha Watanzania vinasaba vyao vikoje na vinaweza kutumikaje katika masuala mazima ya afya huku tukijilinda na magonjwa mbalimbali, "amesema.
Hivyo amesema watanzania wana fursa kubwa sana ikiwa wataweza kuwasaidia hao watalaamu waweze kufanya utafiti wao kwa kina."Tukifanya hivyo kazi itakuwa rahisi na vikao hivi tunavyofanya leo na baadae vitazaa matunda , nimeona leo tunayo fursa adhimu ,sisi ni mabingwa wa kazi hizi, Serikali ikitoa fursa tutafanya kazi kubwa.
"Mashirikiano ya wananchi wote ,mashirikiano ya kuwa na taarifa za kutosha kuhusu vinasaba yatasaidia sana kuleta uelewa wa Tanzania kuona kwamba tunayo fursa tuitumie ,tufanye uchunguzi wa vinasaba vyetu na kuviorodhesha ili visaidie Tanzania yetu lakini pia na dunia nzima,"amesema.
Awali Rais wa taasisi hiyo ya Watafiti na Wanataaluma wa vinasaba vya binadamu Tanzania Dkt. Siana Nkya amesema kongamano hilo limeandaliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Chama mama cha Watafiti na Wanataaluma wa vinasaba vya binadamu Afrika pamoja na mtandao wa watafiti na wanataaluma wa vinasaba vya binadamu Afrika.
Amesema kongamano hilo ni la kitamaduni ambalo linatokea kila mwaka barani Afrika lakini kwa Tanzania ni mara ya kwanza kufanyika, katika historia ya nchi wameandaa kama waandaji wakuu kwa kushirikiana na wadau ambao amewataja." Kwasababu hiyo basi kwetu ni fursa muhimu kwa ajili ya kuchochea harakati za maendeleo ya ukuaji elimu ya vinasaba vya binadamu Tanzania pamoja na matumizi yake hususani kwenye afya.
"Kongamano hilo limepewa jina la Matumizi ya Elimu ya Vinasaba kwa ajili ya kuboresha Afrika, kwa hiyo kila mada inayotolewa hapa inalenga kuleta maboresho kwenye afya kwa waafrika na duniani , Tanzania imechaguliwa kuwa muandaaji wa huu mkutano kwa sababu za kihistoria ,tunajua binadamu wote walianzia Afrika na hususani Afrika Mashariki.
"Na sisi Tanzania ni nafasi muhimu kuundaa na kuushiriki huu mkutano kwasababu si tu ya kihistoria tuliyoijua kawaida lakini historia hiyo ina maana kubwa tunapokuja kwenye habari ya vinasaba vya binadamu.Tunaamini tafiti zinazoendelea za vibasaba vya binadamu hapa Tanzania vitakuwa na mchango mkubwa katika afya hapa Tanzania lakini na duniani kote,"amesema.
Wakati huo huo Mjumbe wa bodi wa Taasisi ya Magonjwa adimu nchini,Balozi Togolani Mavula amaesema taasisi inahusika na magonjwa adimu hasa ya watoto waishio na magonjwa adimu, Balozi Togolani Mavula amesema wao wanashughulika na magonjwa hayo yanaitwa adimu kwasababu yanawapata watu wachache duniani kote na bahati mbaya ni magonjwa ambayo hayana tiba yake bado ni ngumu kupatikana hadi sasa.
Amefafanua , ni magonjwa ambayo asilimia 70 yanatokana na vinasaba, ugonjwa mmoja unaweza kukuta katika watu laki mbili unapata mgonjwa mmoja.Na inakuwa ni ngumu sana kwani hata kutengeneza mashine ya kujua ugonjwa wa mgonjwa kati ya watu lakini mbili hata kiuchumi inakuwa sio kazi rahisi.
"Sisi ni wadau muhimu sana kwa wenzetu hawa wa vinasaba kwani magonjwa yale ili uyatambue yanategemea sana elimu ya vinasaba na tunashukuru wenzetu hawa wameanza hapa Tanzania ,kwanza kufikiria kutoa elimu ya vinasaba , ni sayansi muhimu sana huko tuendako ,huku kwetu imebakia kubishana kujua mtoto ni wa nani , lakini kuna mengi zaidi.
"Wenzetu huko duniani kwa kujua vinasaba vya mtu unaweza kutengeneza dawa inayomfaa kutokana na mahitaji ya mwili wake,kwamba dawa inayonifaa mimi sio lazima imfae mwingine,kila mtu anatengenezewa dawa yake ,lakini dunia inaelekea kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda ,sasa tunaweza kuzungumzia unaweza kuhakiki vinasaba ili kuondoa baadhi ya magonjwa
"Huko tuendako baadhi ya magonjwa tunaweza kuyaepuka, sasa hivi kuna tafiti zinafanyika katika selimundu kwamba hata wana ndoa wanaweza kabla ya kuona wanaweza kuangalia kama kuna uwezekano wa kuzaa mtoto mwenye selimundu au mtoto anapozaliwa unaweza kuangalia kama ana vimelea vile ili kudhibiti madhara yanayotokana na vinasaba hivyo.
"Kwa hiyo sisi tunawashukuru kwasababu tunao watoto wa kutosha ,mmojawapo kwa sasa anakaribia miaka 10 sasa lakini kwa miaka saba lakini haijulikani anaumwa nini ,tunajua kwamba ugonwa wake ni adimu lakini tumeshindwa kugundua ni ugonjwa upi anaumwa , kutokana na kutokuwepo kwa utambuzi, kwa hiyo wanasayansi wanapokutana hasa wa Afrika ni habari njema.
"Wenzetu wa Magharibi, wenzetu wa Asia wamefika mbali sana,sisi waafrika tuko bilioni moja si haba ,si wengi sana lakini sio haba na wenye vinasaba mbalimbali ,vyote vikijulikana na kuhifadhiwa vinaweza kusaidia baadhi ya majawabu ya magonjwa na magonjwa yanayotusumbua.
"Kuna magonjwa mengine sisi vinasaba vyetu vina nguvu dhidi ya magonjwa fulani,wenzetu wanahangaika nayo kama ambavyo na wao wana vinasaba ambavyo vinaweza kukabiliana na magonjwa fulani ambayo kwetu yanatusumbua kwa hiyo ni hatua nzuri ,tunaunga mkono,"amesema.Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar, Mh.Nassor Ahmed Mazrui akizungumza mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kufungua kongamano linaloendelea kufanyika jijini Dar es Salaam la 'Matumizi ya Elimu ya Vinasaba kwa ajili ya kuboresha Afrika' linalowahusu WATAALAM wa masuala ya Vinasaba vya binadamu Tanzania ambao wameungana na wataalamu wenzao wa vinasaba vya binadamu Bara la Afrika kwa ajili ya kujadiliana mambo mbalimbali ya vinasaba katika kuboresha afya za waafrika na dunia kwa ujumla.
Rais wa taasisi hiyo ya Watafiti na Wanataaluma wa vinasaba vya binadamu Tanzania,Dkt. Siana Nkya ( katikati) akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dar,kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar, Mh.Nassor Ahmed Mazrui kuzungumza na Waandishi wa habari,Kushoto ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya Watafiti na wanataaluma wa Vinasaba vya Binadamu Tanzania,Mohamed Zahir
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar, Mh.Nassor Ahmed Mazrui akizungumza jambo na Mjumbe wa bodi wa Taasisi ya Magonjwa adimu nchini,Balozi Togolani Mavula kabla ya kuanza kuzungumza na Waandishi wa Habari
Mjumbe wa bodi wa Taasisi ya Magonjwa adimu nchini,Balozi Togolani Mavula akizungumza mbele ya Waandisha habari (hawapo pichani),akieleza kuunga mkono kongamano la 'Matumizi ya Elimu ya Vinasaba kwa ajili ya kuboresha Afrika',linaloendelea kufanyika jijini Dar es Salaamu
Home
AFYA
HABARI
WATALAAMU VINASABA VYA BANADAMU WAKUTANA KUWEKA MIKAKATI YAO, WATAELEZA FAIDA ZA KUKUSANYA TAKWIMU ZA VINASABA KATIKA AFYA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...