Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAZIRI wa Madini Dotto Biteko amepongeza Mkurugenzi wa kampuni ya Tanzanite Forever Lapidar Ltd, Faisal Juma Shabhai kwa kutengeneza ofisi nzuri za kununulia madini ya Tanzanite kwenye mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Waziri Biteko ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite kwenye ukumbi wa Mazubu Grand Hotel Mji mdogo wa Mirerani.
Ameeleza kuwa mara baada ya Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza biashara ya madini ya Tanzanite, kampuni yaTanzanite Forever Lapidar ilitekeleza mara moja agizo hilo.
“Hao wanaodhani biashara ya madini ya Tanzanite itarejea jijini Arusha wanadanganyana kwani Serikali imeshaamua shughuli zote zitafanyika Mirerani hivyo wafanyabiashara wote wakubwa igeni mfano wa kampuni hiyo kwa kujenga ofisi nzuri,” amesema Biteko.
Mkurugenzi wa Tanzanite Forever Lapidar Ltd, Faisal Juma Shabhai amemshukuru Waziri Biteko kwa kuona juhudi zao za kuwekeza kwenye sekta hiyo ya madini kupitia ofisi yao.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali yetu katika kuhakikisha tunatekeleza wajibu wetu katika biashara hii ya Tanzanite kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu,” amesema Faisal.
Mwenyekiti wa Kamati ya madini ya Tanzanite, Money Yusuph amesema wanatarajia kuandaa tamasha kubwa la Tanzanite la kupandisha madini hayo kileleni mwa mlima Kilimanjaro lengo likiwa ni kuyatangaza zaidi.
Money amesema mgeni rasmi wa tamasha hilo la madini ya Tanzanite anatarajiwa kuwa Waziri wa Madini Dotto Biteko na
tamasha hilo linataandaliwa na wadau wa madini ya Tanzanite watakaohakikisha madini hayo yanafikishwa hadi juu kileleni mwa mlima Kilimanjaro.
"Mgeni rasmi wa tamasha hilo utakuwa wewe mwenyewe Waziri Biteko utakayetuongoza kuupandisha mlima Kilimanjaro na madini yetu yatafikishwa kileleni," amesema Money.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, (Marema) Tawi la Mirerani, Jumanne Nahe amesema shughuli za uchimbaji zimekuwa ngumu hivyo wachimbaji wapatiwe ruzuku za zana za uchimbaji.
"Wachimbaji wengi wamefilisika kwani wenye leseni za uchimbaji madini ya Tanzanite wapo 600 ila wanaochimba wapo 50 hivyo wapatiwe ruzuku za uchimbaji," amesema.
Mmoja kati ya wachimbaji wa madini ya Tanzanite, Shwaibu Mushi amesema eneo tengefu la madini ya Tanzanite lingepaswa kuwa na sheria maalum kuliko kutegemea matamko ya viongozi.
"Sheria ya eneo tengefu iwepo kwa vitalu vyote na pia sheria ya kuchimba kwa mshazari iwepo kwani hii sheria ya kuchimba wima haitekelezeki kwa madini ya vito," amesema Mushi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...