Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MWANAMUZIKI maarufu wa muziki wa dansi Fally Ipupa amewasili nchini Tanzania akiwa na kundi la zaidi ya wanamuziki 35 kwa ajili ya kufanya maonesho katika ukumbi wa Mliman City jijini Dar es Salaam Oktoba 9,2021 na baadae ukumbi wa Malaila katika Jiji la Mwanza Oktoba 13.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Termina III jijini Dar es Salaam amesema anao uzoefu wa kutosha na wa muda mrefu katika muziki wa dansi,hivyo watanzania watarajie burudani ya nguvu kutoka kwake sambamba na nyimbo zake mpya.
" Nimekuja na vitu vingi vipya, kutakuwa na Suprise , hivyo Watanzania watafurahi sana, niwahakikishi mashabiki wa muziki wa dansi watakaokuja Mlimani City na baadae katika Jiji la Mwanza watafurahi,mimi na wanamuziki wangu tumejipanga,tumejiandaa kutoa burudani ,niwaombe tu kateni tiketi mapema,"amesema.
Ameongeza kuwa anatambua hajaja Tanzania kwa zaidi ya miaka 10, hivyo kuna nyimbo nyingi ambazo amezitoa lakini anawaachi mashabiki ndio wataamua wanataka kusikia nyimbo gani kutoka kwake ingawa amejiandaa vya kutosha."Niwahakikishie nitafanya Show ambayo sijawahi kufanya hapa Tanzania,njooni Mliman City siku ya Jumamosi, kutakuwa na Sebene na Rhumba kali."
Kuhusu idadi ya kundi ambalo amekuja nalo ,Fally Ipupa amesema kutoka Paris Ufaransa amekuja na jumla ya watu nane na wengine 24 wataingia usiku wa leo kwa Shirika la Ndege la Ethiopia wakitoa Kinshansa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Prime Time God Kusaga amesema Fally Ipupa tayari amewasili nchini na onesho lake la kwanza litafanyika Jumamosi ya Oktoba 9 katika ukumbi wa Mliman City na baada ya hapo atakwenda Mwanza katika ukumbi wa Malaila Oktoba 13 mwaka huu ambayo itakuwa siku ya mkesha wa Maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Julius Nyerere .
"Maandalizi yamekamilika,tunawaomba mashabiki na wapenzi wa muziki wa dansi,mashabiki wa Fally Ipupa kukata tiketi mapema kwani zimebakia chache kumalizika , tunaamini atafanya Show nzuri na kuutangaza utalii wetu,"amesema Kusaga.
Akizungumzia bei ya viingilio amesema kwa Dar es Salaam ni Sh.100,000 kwa kiti na meza itakuwa Sh.milioni Moja wakati Mwanza kiti itakuwa Sh.50,000 na meza Sh.milioni moja.Msisimko ni mkubwa sana na milango itakuwa wazi kuanzia saa 12 jioni,amesisitiza Kusaga.
Ameongeza kuwa ujio wa Fally Ipupa watanzania wategemee Show kubwa,ya kisasa kwa Dar es Salaam na Mwanza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...