Na Mwandishi wetu, Mirerani

KATIKA maisha imezoeleka kuwa watu wakishafunga ndoa, husherehekea harusi zao kwenye kumbi mbalimbali au majumbani mwao, lakini imekuwa tofauti kwa mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Innocent Abdalah (Arafat) ambaye amesherehekea ndoa yake na watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.

Arafat amefunga ndoa hiyo na Joyce Joseph Oktoba 30, kwenye kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozali Takatifu ya mji mdogo wa Mirerani na kisha kusherehekea harusi hiyo na watoto yatima na wanaoishi mazingira magumu wa kituo cha Light In Africa.

Akizungumza baada ya kufunga ndoa hiyo Arafat amesema Mungu ndiye hupanga kila jambo hivyo anafurahia moyoni kwa kusherehekea na watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.

"Watu wengi husherehekea harusi zao kwenye kumbi kubwa au majumbani kwao ila mimi ninafurahia na watoto hawa wenye uhitaji na ninajisikia faraja mno," amesema Arafati.

Paroko wa Kanisa hilo, Padri Vincent Tendeu amewapongeza maharusi hao kwa kusherehekea ndoa hiyo pamoja na watoto yatima wa kituo hicho cha Light In Africa.

"Ni utukufu kwa Mungu kuwakumbuka watoto yatima, walemavu na wenye mahitaji maalum pamoja na kushiriki chakula, kitendo hicho kinapaswa kuigwa na wengine," amesema Padri Tendeu.

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Anthony Ajemi amesema tukio hilo ni mara ya kwanza kuliona ila jamii inapaswa kuiga hilo ili kuwapa faraja watoto wenye uhitaji maalum.

"Arafati ni maarufu hapa Mirerani lakini yeye hakukusanya michango yao mtu yoyote ili afanye sherehe, hapana alitumia fedha zake kusherehekea harusi yake na watoto yatima," amesema Anthony.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...