Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM,) kimesema hakifurahishwi na kitendo kilichofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaodaiwa kupiga wananchi wa Jimbo la Ushetu mkoani Shinyanga hadi kuwavunja miguu kwa kisingizo cha kuwakamata na mkaa au kuwabambizikia kesi zizizo na msingi.
Akizungumza akiwa katika jimbo la Ushetu Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka amesema Chama chao kinalaani vikali tabia hiyo inayofanywa na watu wa Mamlaka hiyo.
"Kibaya zaidi wanapowafikisha watuhumiwa polisi, hawawapeleki hata mahakamani wanatozwa faini ambazo hazina hata stakabadhi, niwakikishie wananchi Serikali CCM inayongozwa na Rais Samia haitavumilia jambo hili tunasimama upande wenu, kuweni na amani endeleni kutiii sheria bila shuruti,"amesema.
Ameongeza ni vema wakala hao wakatoa elimu ya msingi na taratibu kwa wananchi ili waweze kujua na sio kuwadhalilisha vijana hao kwani wanaweza kutii Sheria bila shuruti."CCM haiwezi kukubali hali hii ya vijana kudhalilishwa,tukitoka hapa nitampigia simu Waziri mwenye dhamana na kuzungumza naye juu ya hili suala waache mara moja kuwadhalilisha vijana,"amesema na kuongeza.
"CCM haitakubali kuona wananchi kwenye maeneo ya hifadhi ya misitu wakiishi kama vile wao ni wakimbizi katika nchi yao. TFS acheni uonevu na unyanyasaji wa wananchi wanaopakana na misitu hususan hapa Jimbo la Ushetu."
Shaka amesema Chama kitaelekeza serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuheshimu vijana ili nao wawaheshimu vizuri na kuacha kuwavunja miguu na kuwadhalilisha.
Aidha anatarajia kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi ,IGP Simon Sirro kuhusu tabia ya baadhi ya askari Polisi katika jimbo la Ushetu kubambikizia wananchi kesi za kukamatwa na bangi hususani kwa vijana na wanawake vitendo vinavyofanywa na baadhi ya askari wasio waaminifu wa Mkoa huo.
"Chama Cha Mapinduzi tutazungumza na IGP leo hii jicho lake liangalie wilaya ya Kahama haiwezekani wananchi wako kwenye nchi huru leo hii wakafanywa wanaishi kama wakimbizi kwa vitu vya kusingiziana na kubambikiziana kesi kubwa na zito,"alisema Shaka.
Amesisitiza CCM hakikubaliani na hali hiyo hata kidogo na wala hakiridhishwi kwa utendaji huo wa baadhi yaO."Nitamtafuta IGP na kuzungumza naYe kuhusu hili kwani wanawake na vijana wanachukuliwa mali zao na kuharibiwa na hawa Askari,"alisema.
Shaka amesema Chama kipo imara na hakikubaliani na Tabia hizo hivyo wanataka kuzimaliza iwe mwanzo na mwisho.
"Tumekuwa tukihubiri amani ,umoja na mshikamano wakati wote lazima wananchi wawe na imani na vyombo vyao vya dola na lazima wote twende pamoja katika safari iliyokusudiwa, "alisema.
Wakati huo huo Shaka amesema suala la ushindi katika Jimbo la Ushetu halina mjadala wanashinda kwa sababu wamekuwa wakitatua changamoto za wananchi hususani kipindi hiki cha awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema tayari mkoa wa Shinyanga una mradi Mkubwa wa maji safi na salama ambao upo katika hatua ya upembuzi yakinifu na upo katika hatua nzuri kutoka ziwa Victoria.
"Rais Samia kawaletea Milioni 400 kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo la upembuzi yakinifu ili kuhakikisha jimbo hilo maji safi na salama yanapatikana kwa uhakika na tatizo la maji kuwa la historia kwa muda mfupi ujao,"amesema na kuongeza.
"Tayari Sh.bilioni sita zimefika kwa Mamlaka ya maji vijijini kwa jimbo hili kuhakikisha miundombinu ya maji inatandikwa kuwafikia wananchi."
Kuhusu maji amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia imetoa Sh.bilioni 72 kwaajili ya ujenzi wa barabara na ukarabati Stendi za mabasi na madampo.
Shaka amesema upande wa elimu kwa mkoa wa Shinyanga Rais Samia kila mwezi anatoa sh.Milioni 591 kwaajili ya kuwalipia watoto ili wapate elimu bure bila malipo."CCM inakazi moja tu kuleta maendeleo katika jimbo la Ushetu ambapo kwenye sekta ya afya Milioni 750 za tozo ya miamala zimeletwa katika mkoa huo kwa ajili ya afya mkoani humo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...