CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimesema kwa tathmini ambayo wameifanya wana uhakika wa ushindi katika Jimbo la Konde, Jimbo la Ushetu na kata zote tatu kwa sababu imesimamisha wagombea wenye sifa za uongozi.
Kimesema wanafahamu mahitaji ya wananchi wao, wanaokubalika na wapiga kura wa rika zote, zaidi chama kimefanya kampeni za kisayansi sana zilizowafikia wapigakura wengi kuliko chama chochote iliyopokewa kwa hamasa na matumaini makubwa.
Tathimini hiyo imetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa kampeni za Chama hicho tangu Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) ilipotangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo Septemba 10, 2021.
Uchaguzi huo utafanyika katika jimbo la Konde kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge Mteule wa jimbo hilo Shekha Mpemba Faki kwa sababu za kifamilia kama alivyoeleza kupitia barua yake na Jimbo la Ushetu kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Elias John Kwandikwa na Udiwani katika Kata 9 za Tanzania Bara utakaofanyika Oktoba 9, 2021.
Shaka amesema utekelezaji mzuri wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 unaofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika maeneo yote hayo kuanzia uboreshaji wa huduma za kijamii kama afya, elimu, maji safi, nk ni miongoni mwa mambo yaliyowapa wananchi imani kubwa kwa chama hicho.
"Mpaka sasa katika kata 9 zilizotangazwa kurudia uchaguzi, kata 6 tumepita bila kupingwa ambazo ni Mbuyuni mkoani Dar es Salaam, Dogo mkoani Manyara, Udugu mkoani Njombe, Ndembezi mkoani Shinyanga, Lingwa mkoani Singida na Kileo mkoani Kilimanjaro. Hivyo ni kata tatu tu ndizo zitafanya uchaguzi siku ya tarehe 9 Oktoba, 2021 na ambazo tunauhakika wa kushinda kwa sababu tulizozieleza hapo juu.
"Tunatoa mwito kwa wanachama wetu na wananchi wa maeneo ya Jimbo la Konde, Jimbo la Ushetu na Kata ya Neruma Bunda mkoani Mara, Lyowa Kalambo mkoani Katavi na Vumilia Urambo mkoani Tabora kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 9 Oktoba, 2021 asubuhi mapema kuwachagua wagombea wanaotokana na CCM, baada ya kupiga kura warejee majumbani kuendelea na shughuli zao wakati wakisubiri kusherehekea ushindi,"amesema.
Ameongeza kwamba Chama Cha Mapinduzi kina matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi katika majimbo yote ya Konde, Ushetu na kata tatu zinazorudia uchaguzi. Aidha CCM itakuwa tayari kupokea matokeo yoyote kwani hiyo ndiyo demokrasia.
Amefafanua kwa mujibu wa ratiba ya kampeni za uchaguzi huo mdogo CCM ilifanya kampeni zake za ubunge jimbo la Konde lililopo wilaya ya Micheweni, mkoa wa Kaskazini Pemba, Jimbo la Ushetu lililopo wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga vivyo hivyo kwenye kata zote tatu ambazo ni Neruma iliyopo wilaya ya Bunda mkoani Mara, Kata ya Lyowa iliyopo wilaya ya Kalambo mkoa wa Katavi na Kata ya Vumilia iliyopo Wilaya ya Urambo mkoa wa Tabora kikamilifu.
"CCM inawashukuru sana wanachama wake na wananchi katika maeneo yote hayo kwa namna walivyojitoa na kushiriki kampeni za wagombea wetu kwa hamasa kubwa, amani na utulivu,"amesema Shaka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...