Ugonjwa wa Corona (UVIKO-19) umesababisha changamoto nyingi duniani katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, uchumi, usafirishaji, maji na utalii, hivyo dunia imetakiwa kuchukua changamoto hizo kama funzo ili kujipanga upya na namna ya kukabiliana na majanga ya mlipuko.

Hayo yemeelezwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) alipokuwa anahutubia katika sherehe za kuadhimisha Miaka 76 ya Umoja wa Mataifa (UN DAY) zilizofanyika leo jijini Dodoma kwenye viwanja vya Nyerere Square.

Dkt. Tax alisema kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu “Kujijenga tena kwa kujenga mifumo ya afya bora” ni kielelezo cha wazi kuwa dunia haina budi kushirikiana ili kujenga mifumo madhubuti ya afya yenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko. Lengo la mifumo hiyo ni kuhakikisha kuwa nchi hazipati athari kubwa zinazosababishwa na majanga kama hili la mlipuko wa UVIKO-19.

Dkt. Tax aliushukuru Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano wake katika sekta mbalimbali nchini na kuuahidi umoja huo na wadau wengine wa maendeleo kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana nao katika kukabiliana na janga la Corona. Alifafanua kuwa Serikali itaendelea kufuata miongozo yote inayotolewa na Shirika la Afya Duniani pamoja na kujenga mfumo imara wa afya wenye kuhakikisha vituo bora vya afya, watumishi wa kutosha, vitendea kazi, dawa na miundombinu mingine ili kutoa huduma bora za afya nchini.

Alisema Serikali ilishaweka mikakati ya utekelezaji wa haya yote katika Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma hivi karibuni.

Alihitimisha hotuba yake kwa kuwahimiza wananchi kutumia fursa ya chanjo zilizopo nchini, kwa kuwa chanjo hizo zinapatikana kwa tabu na hadimu duniani.

Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Ziatan Milisic alisema kuwa kufanyika kwa maadhimisho hayo, inaashiria kuwa Umoja wa Mataifa una dhamira ya dhati ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali kama za afya, elimu mazingira ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...