Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MAAFISA Watendaji wa Kata katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya chanjo ya ugonjwa wa Uviko-19 unaosababishwa na virusi vya Corona katika maeneo yao.
Wito huo ulitolewa na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Lucas Mbise alipokuwa akifungua kikao kazi cha tathmini ya mkataba wa Lishe kwa Maafisa Watendaji wa Kata kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Afya Jiji la Dodoma katika hafla ya kusaini nyongeza ya Mkataba wa Lishe kwa mwaka 2021-2026.
Mbise alisema kuwa Rais alipoingia madarakani aliunda kamati ya kumshauri juu ya ugonjwa wa Uviko-19. Alisema kuwa baada ya ushauri huo akatoa maelekezo ya utaratibu wa chanjo kwa hiari na akaizundua chanjo hiyo yeye mwenyewe.
“Maelekezo ya sasa wataalam wapite kwenye maeneo yetu kutoa elimu na wewe kama kiongozi unawajibu wa kutoa elimu hiyo ili iwafikie wananchi wote. Tusimame kama viongozi, tutekeleze wajibu wetu, ila maamuzi ya kuchanja au kutokuchanja tuwaachie wananchi wetu” alisema Mbise.
Kwa upande wa mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Gerald Ruzika alisema kuwa Maafisa watendaji wa kata wana wajibu wa kusimamia suala la utoaji elimu ya chanjo ya ugonjwa wa Uviko-19 kwa umakini.
“Mkisoma Sera ya Utumishi wa Umma aya ya 32; watumishi wote wanafanya kazi kwa niaba ya Rais. Huwezi kupingana na maagizo ya Rais. Hivyo, lazima tuwe mabalozi wa mambo mazuri yanayoanzishwa na serikali. Utakuwa afisa wa ajabu kutokukubaliana nayo. Ni bora uchukue uamuzi wa kujiuzuru. Sisi tunabeba dhamana ya wengi wanaotuamini” alisema Ruzika.
Mwalilishi wa Mkurugenzi wa Jiji, Gerald Ruzika akifafanua jamboPicha LIshe Backgroud: Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Lucas Mbise (wa pili kulia) na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Gerald Ruzika (kushoto) walisikiliza mada
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...