UTEKELEZAJI wa mapitio ya mpango wa upangaji wajasirimali wadogo (Machinga) katika maeneo rasmi ya kufanyia biashara, mkoani Ruvuma utafanyika kwa kipindi cha miezi mitatu.
Haya yamesemwa na
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati anataja maazimio kwenye kikao cha
mkakati wa kuwapanga Machinga katika maeneo ya kufanyia biashara kilichofanyika
kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Kikao hicho
kimeshirikisha wadau kutoka Halmashauri
zote za Mkoa wa Ruvuma wakiwemo wakuu wa wilaya,wenyeviti wa Halmashauri,
makatibu Tawala,Kamati ya ulinzi Mkoa wa Ruvuma,viongozi wa Machinga ngazi ya
Mkoa,wakurugenzi wa Halmashauri, wataalam mbalimbali na viongozi mbalimbali wa
Taasisi za serikali zikiwemo TRA, SOUWASA, TANROADS, TARURA,RUWASA na LATRA.
Brigedia Jenerali
Ibuge amekitaja kipindi cha utekelezaji mkakati huo kuwa ni kuanzia Mwezi
Novemba,Desemba na Januari 2022 na kwamba wameazimia ifikapo Januari 30 mwakani
utekelezaji wa kuwapanga Machinga uweke
umekamilika.
“Ili kuhakikisha
zoezi hilo linafanikiwa kwa weledi,tunaazimia itakapofika Novemba
30,majadiliano ya uboreshaji kwa kuzingatia uwakilishi wa makundi yote yakiwemo
viongozi wa Machinga yatakuwa yamekamilika hivyo tutakutana tena hapa kama
wadau ili kupata mrejesho’’,alisisitiza RC Ibuge.
Ameagiza zoezi la
upangaji maeneo lishirikishe viongozi waliochaguliwa na Machinga kwenye maeneo
yao ili kuleta umoja na ushirikishwaji katika makundi yote.
Hata hivyo ametahadharisha
kuwa uboreshaji wa mpango wa upangaji Machinga,pale ambapo utawahusisha
wafanyabiashara wakubwa wasiokuwa Machinga,ni lazima kuhusisha vikao vya pamoja
nao ili kutoingia mwenye migogoro.
Mkuu wa Mkoa ameagiza
Halmashauri zote nane mkoani Ruvuma kuhakikisha kuwa,baada ya
makubaliano,waweke miundombinu wezeshi kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya
Machinga ili kuweza kwenda sanjari na mwisho wa utekelezaji wa kuwapanga
Machinga kwenye maeneo yao.
Ameziagiza Taasisi
zote kwenye Halmashauri zikiwemo TRA, TARURA, RUWASA, TANESCO, TANROADS na
LATRA washiriki kikamilifu kuwezesha maeneo muhimu ya kuwekewa miundombinu
wezeshi ili kuwezesha uhamaji na
upangaji wa Machinga katika maeneo rasmi ya biashara.
Hata hivyo
amesisitiza kuwa kutokana na upekee wa zoezi la upangaji Machinga,juhudi za
makusudi zifanyike kuhakikisha mabaraza ya Biashara ya Halmashauri na Manispaa
yawe yamepata taarifa na kufanya majadiliano ya utekelezaji wa mpango wa
Halmashauri husika na viongozi wa Machinga kabla ya kikao cha marejeo.
RC Ibuge ameutaja
upangaji wa Machinga kwenye maeneo rasmi kwa Mkoa wa Ruvuma kuwa ni fursa kubwa
kwa kuwa Halmashauri zina maeneo makubwa ambayo yanatakiwa kuwekewa miundombinu
kwa ajili ya kuwawezesha Machinga kufanya biashara bila shida.
Akizungumza kwenye
kikao hicho Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Ruvuma Salum Masamaki ameishukuru
serikali kwa kuwapangia Machinga maeneo
rasmi ya kufanyia biashara ambapo amesema sasa wataweza kufanya biashara zao
kwenye maeneo yenye utulivu na kwamba wapo tayari kutoa ushirikiano katika
utekelezaji wa zoezi hilo.
Naye Mwenyekiti wa
CCM Mkoa wa Ruvuma Ndugu Odo Mwisho ameipongeza serikali kwa kutoa fursa ya
kuwapangia Machinga maeneo rasmi ya biashara ambapo ametoa rai kwa viongozi wa
Machinga Mkoa kuzunguka katika Wilaya zote
ili kutoa elimu kwa Machinga kuhusu mpango huo wa serikali wenye tija kwao.
Mkuu wa Wilaya ya
Nyasa Kanali Laban Thomas akizungumza kwenye kikao hicho ametoa rai kwa
Machinga kuondoa hofu kwenye utekelezaji
wa mpango huo ambapo amesisitiza Machinga wana thamani kubwa kwa sababu
popote watakapopangiwa na serikali, wanunuzi watafuata bidhaa zao.
Pololet Mgema ni Mkuu
wa Wilaya ya Songea ametoa rai kwa viongozi wa Machinga Mkoa wa Ruvuma,
kufuatilia muundo wa Taasisi yao yenye viongozi kuanzia ngazi ya kitaifa,ili
kujua katiba yao inavyoelekeza ili kutekeleza
majukumu yao kwa maslahi ya Machinga
wote.
Mkoa wa Ruvuma
unakadiriwa kuwa na wajasiriamali wadogo (Machinga) wapatao 28,000 ambao
wanafanya biashara zao kwenye maeneo mbalimbali ya Halmashauri nane za Mkoa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...