Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha 

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela leo tarehe 23.10.2021 amefungua rasmi zoezi la ukaguzi wa vyombo vya moto kuelekea maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Arusha kuanzia tarehe 15.11.2021 hadi tarehe 20.11.2021.

Katika ufunguzi huo Mhe. Mkuu wa Mkoa mbali na kupongeza Jeshi la polisi kupunguza matukio ya ajali za barabarani na ubunifu wa kwenda katika maeneo ya wanaomiliki idadi kubwa ya vyombo vya moto kwa ajili ya kukagua vyombo vyao, amewapongeza wadau wa usalama barabarani hususani madereva kwa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya ukaguzi wa vyombo vyao.

Aidha amesema ni muhimu Wananchi waendelee kuelimishwa kuhusiana na sheria za usalama barabarani na kukemea vitendo vya rushwa kwa Askari wachache ambao wanachafua taswira ya Jeshi la Polisi.

Alimaliza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza maadhimisho hayo kitaifa yafanyike Mkoa wa Arusha, hivyo akatoa wito kwa wadau wa usalama barabarani kushikama na kujitoa kwa pamoja  ili kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanyika kwa hali ya amani na utulivu.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo wakati akimkaribisha Mkuu wa Mkoa alisema kama Watumiaji wa vyombo vya moto watafuata kauli mbiu ya utii wa Sheria bila shuruti watapunguza ajali nyingi za barabarani ambazo zimepelekea watu wengi kupoteza maisha, ulemavu pamoja na uharibu wa vyombo vya moto.

Awali akitoa taarifa fupi kuhusiana na maadhimisho hayo Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi Solomon Mwangamilo amesema lengo la maadhimisho hayo ni kutoa nafasi kwa baraza la usalama barabarani kufanya tathmini ya jumla kwa mwaka mzima kuhusiana na usalama wa watumiaji wote wa vyombo vya moto, kuangalia maeneo ambayo yanapelekea ajali nyingi za barabarani na kuja na mikakati ya kupunguza ajali izo.

Aliendelea kusema katika wiki hiyo watatoa elimu ikiwa ni pamoja na kukagua vyombo vyote vya moto vilivyopo mkoani Arusha, ambapo amesema wametenga maeneo tofauti kwa ajili ya zoezi hilo kwa kuzingatia ukubwa wa Jiji, ambapo alisema litafanyika katika vituo vya Polisi, viwanja vya Soweto na kwa upande wa wanaomiliki idadi kubwa ya vyombo vya moto watapeleka Wakaguzi wa magari kwenda kufanya ukaguzi katika maeneo yao baada ya kupokea maombi lengo likiwa ni kupunguza ucheleweshwaji wa utoaji huduma.

Ufunguzi huo umehudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha Bwana Zelote Steven pamoja na viongozi mbalimbali.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...