Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako  amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara kufanyia kazi  kikamilifu yale yote ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa akiyasemea katika hotuba zake, maelekezo na mipango ya Taifa kwa kuwa ana lengo la kuendelea kujenga uchumi na kuondoa kero za wananchi.

Waziri Ndalichako amesema hayo Jijini Dar es Salaam katika kikao cha Mawaziri wa Elimu Bara na Zanzibar na Watendaji pamoja na Bodi ya Tume ya Taifa ya UNESCO na kuzitaka Taasisi zote kutekeleza majukumu yake kwa wakati na weledi mkubwa kwa lengo la kutoa matokeo chanya.

“Tunamshukuru sana Mhe Rais kwa kutoa kipaumbele kwenye elimu, ametoa fedha ambazo zitawezesha kujenga madarasa elfu 15 kwa mpigo, madawati zaidi ya laki nne kwa mkupuo,  kukamilisha VETA  32, kujenga kumbi za mihadhara kwenye vyuo 17 vya ualimu, kununua vifaa vya kufundishia kwenye vyuo vya maendeleo ya wananchi, kuongezea vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa watoto wenye mahitaji maalum, lakini pia tunaendelea kunufaika kupitia sekta nyingine kama  maji yatakapowekwa kwenye mikoa wilaya hakuna shaka shule  na Vyuo vyetu vitanufaika ” amesema Prof Ndalichako.

Akizungumzia majukumu ya Tume ya Taifa ya UNESCO Prof Ndalichako amesema Tume hiyo ina majukumu mengi na mapana ikiwemo kusimamia amani ya dunia na kwamba katika kipindi hiki ambacho Mhe. Rais anasisitiza masuala ya amani, umoja na utulivu ni vizuri Tume hiyo ikafahamu kwamba hilo pia ni jukumu lao kwani huwezi kuwa na amani ya dunia kama hakuna amani ya taifa moja moja.

“Nafahamu mnakuwa na program ambazo zinaanzishwa kwa ajili ya wanawake, vijana, viongozi wa dini, wanasiasa na wahabari zenye lengo la kutoa elimu ambayo inahamasisha amani na usalama kwa maslahi mapana ya nchi, ni vizuri mkajua mna jukumu la kuendelea kuhamasisha na kulinda amani na utamaduni wetu,” amesema Prof Ndalichako.

Pia Prof Ndalichako amewakumbusha wajumbe wa Bodi ya Tume ya UNESCO kuwa wana jukumu la kuendelea kuangalia maeneo ya utalii yanayoendana na urithi wetu yanayofaa kutambulika kwani Rais sasa anaendelea kusisitiza suala la utalii  kwani ni moja ya sekta muhimu ambazo zinaniua uchumi wetu.  

“ Rais amefanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi yetu kupitia Royal Tour ameonesha njia, sasa Mwenyekiti tumuunge mkono Rais wetu sisi kama Tume ambayo tumepewa jukumu la kuangalia hayo maeneo kuhakikisha yanahifadhiwa vizuri, kuyafanyia tathmini kwa weledi kama bado yapo kwenye hadhi yake tukitambua yana mchango katika kuongeza utalii katika nchi yetu lakini kuifanya nchi kujulikana katika ramani ya Dunia kutokana na vivutio vilivyopo,” amesema Waziri Ndalichako

Aidha Prof Ndalichako ameitaka Bodi ya Tume ya UNESCO kuhakikisha Tume inajitangaza kazi inazofanya, ili tuweze kutambulika na mchango wake kuonekana ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Simai Mohamed amesema ni vizuri Bodi ya Tume ya UNESCO kuangalia maeneo ya urithi na kuweza kuishauri Serikali ili kuyaweka maeneo hayo katika urithi wa nchi yetu kwani yakiachwa yanaweza kupotea na kufutika katika urithi wa nchi yetu.  

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya UNESCO Prof. Elifaz Tozo Bisanda amemuahidi Waziri Ndalichako kuwa Bodi anayoisimamia itafanyia kazi maelekezo yote aliyotoa ikiwemo kutangaza Tume ya UNESCO ili  ijulikane pamoja na kuendela  kusimamia majukumu mengine yote ya Tume kulingana na maelekezo ya viongozi hao.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizungumza katika kikao cha Mawaziri wa Elimu Bara na Zanzibar watendaji na Bodi ya Tume ya UNESCO kilichofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohamed Said akizungumza katika kikao cha pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako,  Watendaji na Bodi ya Tume ya UNESCO kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Tume ya Taifa ya UNESCO baada ya kikao cha pamoja kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...