Charles James, Michuzi TV
TANZANIA imeweka wazi kuwa itashiriki kikamilifu katika majadiliano ya masuala yenye maslahi mapana kwa Nchi na kuweka msimamo wake katika mambo Saba.
Msimamo huo ni katika Rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mkataba na makubaliano ya Paris, Kujenga uwezo, Kilimo na Mabadiliko ya Tabia Nchi, Uendelezaji na usambazaji wa Teknolojia, Mchango wa Taifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya TabiaNchi, Upunguzaji Gesijoto kwa kutumia biashara na Jinsia na Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo wakati wa mkutano wake na wandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu msimamo wa Tanzania kwenye majadiliano ya mkutano wa 26 wa Nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.
Jafo amesema mkutano huo utafanyika jijini Glasgow, Scotland kuanzia Oktoba 31 mpaka Novemba 12 mwaka huu na utahudhuriwa na wajumbe takribani 3,000 kutoka Nchi mbalimbali duniani wakiwemo Wakuu wa Nchi, Mawaziri na Wataalamu waliobobea katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Amesema mkutano huo unafanyika wakati ambao Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa duniani likiwa limetoa taarifa inayothibitisha kuwepo kwa ongezeko la joto katika uso wa Dunia.
"Athari hizo ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kulikosababisha kisiwa cha Maziwe Wilaya ya Pangani na kisiwa cha Fungu la Nyani Wilaya ya Rufiji kumezwa na maji ya bahari, Aidha katika msimu wa mwaka 2019/20 mvua zilisababisha kuongezeka kwa kina cha maji kwenye Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.
Serikali imekua ikitumia fedha nyingi ili kukabiliana na athari hizi ambazo zinatishia kurudisha nyuma juhudi za Serikali za miongo kadhaa za kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa watu wake," Amesema Waziri Jafo.
Akielezea msimamo wa Tanzania katika mkutano huo, Jafo amesema kwa mujibu wa mkataba Nchi zilizoendelea ziliahidi kutoa Dola za Kimarekani Bilioni 100 kila mwaka ifikapo 2025 ili fedha hizo ziwezeshe Nchi zinazoendeleaa kama Tanzania kuweka mipango na mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Eneo lingine ni la kujengewa uwezo ambapo amesema Nchi kama Tanzania ili ziweze kujiimarisha kwa ufanisi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi zinahitaji kujengewa uwezo wa kutekeleza majukumu yake kama ilivyobainishwa kwenye mkataba wa makubaliano ya Paris.
" Msimamo mwingine ni kuhusu Kilimo na Mabadiliko ya Tabianchi, kumekua na maoni kinzani kati ya Nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuhusu kujumuisha sekta ya kilimo katika sekta zinazotakiwa kupunguza uzalishaji joto.
Makubaliano ya Paris yanazitaka Nchi zilizoendelea kuziwezesha Nchi zinazoendelea kutumia teknolojia mpya na za kisasa ambazo zitasaidia kuongeza uwezo wa Nchi hizo kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi na kupunguza uzalishaji wa Gesijoto," Amesema Jafo.
Home
HABARI
TANZANIA YAWEKA WAZI MSIMAMO WAKE KWENYE MKUTANO WA WANACHAMA WA MKATABA W UN KUHUSU MABADILIKO YA TABIANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...