Na Amiri Kilagalila,Njombe
Serikali wilayani Njombe imesitisha kuendelea na uwekezaji wa zao la Vanilla katika kijiji cha Idunda wilayani humo mpaka pale itakapojiridhisha na uwekezaji huo unaofanywa na kampuni ya Vanilla International kwa kuwalimia na kuwapandia mashamba watu mbali mbali nchini katika eneo hilo.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Gwakisa Kasongwa baada ya kukagua uwekezaji wa vitalu unaoendelea katika eneo hilo kutokana na kupokea malalamiko kwa baadhi ya wananchi juu ya uwekezaji huo.
"Nitoe wito kwa wananchi ambao wanakusudia kuwekeza kusubiri kwanza kuendelea na uwekezaji uliopo hadi serikali itakapojiridhisha ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza"alisema Kissa Kasongwa
Miongoni mwa mambo ambayo serikali inaendelea kujiridhisha ni pamoja namna kampuni hiyo inavyopata ardhi kwa wananchi na Kijiji,watu waliowekeza fedha kwa ajili ya kulimiwa vitalu na gharama zao pamoja na namna kampuni hiyo inavyofanya kazi.
Hata hivyo serikali imesema inahitaji kujiridhisha zaidi na muda wa kilimo hicho kwa kuwa matangazo ya kampuni yanaeleza kuwa mkulima ataanza kunufaika na zao hilo miezi saba tangu kuoteshwa mmea maelezo yanayokinzana na mwekezaji huyo kwa viongozo wa serikali alivyodai kuwa mkulima ataanza kunufaika baada ya miaka miwili au mitatu toka mche ulipopandwa.
Vile vile licha ya zao hilo kuonekana kuwa ghari duniani kutokana na thamani yake serikali imeeleza kuhitaji kujiridhisha na matangazo ya mwekezaji huyo anayedai kuwa kilo moja ya Vanilla inauzwa mpaka milioni moja tofauti na maeneo mengine nchini ambayo imetajwa kuuzwa mpaka elfu arobaini kwa kilo.
Hivi karibuni mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya pia alifika katika uwekezaji huo na kumuagiza mkurugenzi wa kampuni ya Vanilla International bwana Saimon Mkondya, Kupeleka taarifa za uwekezaji wake ofisini kwake na kueleza kuwa uwekezaji huo unatakiwa kuzingatia sheria.
Rubirya pia alimtaka mkurugenzi huyo kuboresha makazi ya wafanya kazi wanaosaidia shughuli za mashamba hayo ili kuwahakikishia usalama wao siyo ilivyo kwa sasa wanaishi kwa wasiwasi.
Naye kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Njombe Hamis Issa alitoa wito kwa wakulima waliowekeza fedha zao eneo la kijiji cha Idunda kwenye kilimo cha Vanilla kupitia kampuni ya Vanilla International kuhakikisha wanakwenda kutembelea maeneo yao mara kwa mara ili kujiridhisha na mashamba yao.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni hiyo bwana Saimon Mkondya ameileza serikali kuwa yupo tayari kufikisha taarifa za uwekezaji wake.
Serikali ya mkoa wa Njombe imesema inakubaliana na uwekezaji wa zao hilo lakini wawekezaji wake wanatakiwa kufuata taratibu za serikali kwa kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa ili kujiridhisha na kuchukua tahadhari baadae isije kuanza migogoro dhidi ya wakulima.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...