*************************
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
* Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa tamko la Serikali siku ya kilele cha maadhimisho hayo kimataifa Oktoba 13
KAMPENI
Ya elimu kwa Umma kuhusu uelewa wa masuala ya maafa imezunduliwa rasmi
leo Oktoba 7 hadi siku ya kilele Oktoba 13 ambapo ulimwengu utaadhimidha
siku hiyo kwa ajili ya kukuza utamaduni wa usimamizi wa maafa kimataifa
na kitaifa ili kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na
kujiandaa katika kuyakabili na kurejesha hali katika ubora zaidi baada
ya majanga hayo kutokea.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa
kampeni hiyo leo jijini Dar es Salaam Katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu;
Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Tixon Nzunda
amesema maadhimisho hayo ya kitaifa yamejikita katika utoaji wa elimu
kwa umma ili kuhakikisha jamii inatambua aina ya majanga na vyanzo
vyake, madhara ya maafa, kupunguza athari zake na namna ya kujiandaa
katika kuyakabili na tamko rasmi la Serikali litatolewa siku ya kilele
na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.
Nzunda amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni;
"Kwa
Umoja Wetu.....Tunaweza Kuokoa Dunia." Ni fursa kubwa ya kutambua
umuhimu wa ushirikiano baina ya Serikali na wadau wa kimataifa katika
hatua za kuzuia na kupunguza hatari na madhara ya maafa katika mifumo ya
maisha, afya, uchumi, elimu, jamii, utamaduni, miundombinu na
mazingira.
Amesema kuwa elimu hiyo ya uelewa kwa umma kuhusiana
na majanga itatolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo maelezo ya ana kwa ana
kwa wananchi, vipindi vya luninga, redio, vipeperushi vya ufafanuzi wa
maafa na hatua za kuchukua pamoja jumbe katika mitandao ya kijamii.
"Maonesho
ya wazi yatafanyika katika viwanja vya Mazania, Chato Mkoani Geita
kuanzia Oktoba 9 hadi 13 mwaka huu, Dodoma yatafanyika katika viwanja
vya Nyerere Square kuanzia Oktoba 11 hadi 13 na vipindi vya redio na
luninga vitafanyika kuanzia leo hadi siku ya kilele Oktoba 13 na
wataalam mbalimbali watatoa elimu katika sekta mbalimbali ikiwemo maafa,
hali ya hewa, kilimo, ardhi, nishati, Zima moto, shirika la Msalaba
Mwekundu Tanzania, mashirika ya kimataifa na Umoja wa mataifa, Asasi za
kiraia na vyuo vikuu." Amesema.
Nzunda amesema, Serikali imeandaa
mpango wa kukabiliana na maafa katika halmashauri 20 na kwa kuzingatia
wajibu wa sekta katika usimamizi wa maafa na huduma za kibinadamu
imeandaa mpango na miongozo ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika
sekta mbalimbali ikiwemo mpango wa kukabiliana na dharura katika sekta
ya afya, mwongozo wa huduma ya msaada wa kisaikolojia na kijamii kwenye
maafa, mpango wa dharura wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa sekta
ya usafiri wa anga, mpango wa dharura wa kujiandaa na kukabili mlipuko
wa virusi vya Ebola pamoja na mwongozo wa utendaji wa kituo cha
operesheni na Mawasiliano ya dharura.
Vilevile ameeleza kuwa
Serikali itaendelea kuboresha Sera, Sheria na kuandaa mikakati kwa lengo
la kuimarisha mfumo wa uratibu na usimamizi wa maafa nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...