Na John Walter-Manyara
Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amesema ucheleweshaji wa wananchi kupata ufumbuzi wa mashauri ya ardhi mkoani humo unatokana na baraza la Ardhi la Nyumba la wilaya ya Babati ambalo kimsingi linaongoza kuwa na mashauri mengi ya migogoro ya ardhi kuongozwa na Mwenyekiti kutoka mkoa wa Arusha na kuhudumia kwa siku mbili kwa wiki jambo ambalo ameomba serikali kulipatia ufumbuzi.
Aliyasema hayo wakati akikabidhi taarifa ya mkoa kwa mawaziri wanane wa kisekta wakiongozwa na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi wakiwa mkoani humo leo katika mwendelezo wa ziara ya mikoa 10 kutoa matokeo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 920 ulioanzia mkoani Dodoma.
Alisema vyanzo vya maji kupitia miradi ya maji ya RUWASA na Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Babati(BAWASA) vimekuwa havitoshelezi kwa matumizi ya majumbani, viwandani na kunyeshea mifugo ambapo ni sehemu ya kuwepo kwa migogoro ya ardhi ya mara kwa mara.
"Wananchi wa mkoa huu walikuwa wakisubiri ujio wanu mawaziri ili kutoa utatuzi wa migogoro ya mara kwa mara ya ardhi kati ya wananchi na hifadhi, wananchi na wawekezaji pamoja na wananchi na wakulima kutokana na baraza hilo kushindwa kutatua mashauri kwa wakati".Alisema Mkuu wa Mkoa.
Kwa mujibu wake mkoa wa Manyara una upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo wahandisi katika halmashauri zote za wilaya ambapo ameiomba wizara ya TAMISEMI kutatua tatizo hilo ili fedha zinazoendelea kutolewa na serikali za miradi ya maendeleo ziweze kusimamiwa kikamilifu na kuwafikia walengwa.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wiliam Lukuvi alisema mkoa wa Manyara kero kubwa ni pori la akiba la Mkungunero lililopo wilayani Kiteto ambapo kwa kipindi kadhaa amekuwa akijibu maswali mengi kuhusiana na pori hilo ambapo aliagiza timu iliyopo chini ya wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na watu wa wizara ya Maliasili kwenda kufanya uhakiki wote wa kutumia GN za mikoa,wilaya na vijiji .
"Mkungunero hii ina historia ya mikoa miwili ya Manyara na Dodoma ,hivyo ndani ya Serikali tumeamua tutafakari upya juu ya muundo na ramani ya Mkungunero mpaka tulipokia leo"alisema Lukuvi.
Lukuvi alisema katika ziara hiyo ya mkoani Manyara wamekuja kushughulikia sehemu ya matatizo ya vijiji 975 vinavyohusiana na mkoa wa Manyara na yale mengi wanayoyajua ya mashamba,viwanja na mipaka ya vijiji hayo wataendelea kwa utaratibu wao.
" Ujio wetu huu sio wa kumaliza kila kitu hapana tumekuja kushughulikia kila mkoa na kutoa majibu ya maeneo tu yaliyo ndani ya maeneo ya vijiji 975 lakini mengine tutaendelea kushughulikia kwa utaratibu wetu"alisema Lukuvi
Ziara hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu migogoro ya matumizi ya Ardhi kwa vijiji ambavyo wananchi wake walivamia maeneo ya Hifadhi za Misitu, Mashamba na Mifugo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...