MKE wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib amewahimiza wanawake nchini kufanya kazi kwa moyo wa kujitolea na uwajibikaji ili kufikia mustakbali bora wa kuiongoza jamii na Taifa kwa ujumla.

Mama Zainab ameyasema hayo leo katika Ukumbi wa Jimbo la Ziwani, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa kusini Pemba, wakati akiongea na akinamama wa Chama cha ACT-Wazalendo.

Amewasihi wanawake juu ya dhana ya mshikamano na kuvumiliana ili kuyafikia malengo ya uzalendo na kujiendeleza katika nyanja tofauti za kimaisha zikiwemo za elimu, biashara na kuweza kupambana na wimbi la umasikini.

Akiongelea juu ya umuhimu wa wanawake kushika nafasi za uongozi, Mama Zainab amesema ipo haja ya kujitokeza kupitia fursa na njia mbali mbali zikiwemo za kuchukua fomu kupitia vyama na jumuiya zinazowaunganisha ili pia kuhakikisha dhamira hizo zinatekelezwa.

Mama Zainab ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa Hafla hiyo, amewahimiza wanachama waliojitokeza kuchukua kadi za uanachama na pia fomu za uongozi, kusimamia vyema falsafa na misingi bora ya kuwaongoza watu ikiwemo maadili mema.

Akitilia mkazo umuhimu wa kufuata maadili katika kuwaongoza watu Mama Zainab amesema, “jamii inahitaji akinamama viongozi lakini watakaoheshimu misingi ya umoja, uaminifu na watakaoendeleza mshikamano, badala ya kuwagawa na kuwabagua watu kwa kuendekeza maslahi binafsi”.

“Pia nakuhimizeni tuendeleze umoja na mshikamano, tabia ya kusamehe na kusameheana ili kuifikia dhamira ya uzalendo na kufanya kazi kwaajili ya Taifa letu”, amesisitiza Mama Zainab.

Katika ziara yake hiyo, Mama Zainab na ujumbe wake waliweza kuzitembelea familia na kuonana na watoto yatima ambao amewapatia misaada mbali mbali ikiwemo ya vyakula, sabuni na pempas kwa watoto wachanga,na wasiojiweza.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Mke wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, Bi Awena Sinani Masoud amesema kuwa viongozi wa jumuiya, taasisi na vyama vya siasa, wakiwemo wa ACT-Wazalendo wanao wajibu wa kuwafikia wananchi na wanachama katika ngazi zote ili kuwajengea uelewa na moyo wa kujitolea katika kufanikisha maendeleo.

Bi.awena amewataka wanawake wa chama hicho kuepuka mitafuruku na migogoro inayotokana na kutanguliza maslahi binafsi, ili kuwa waalimu bora wa siasa katika Taifa, kwa kutekeleza dhana za umoja, ukweli na uwazi, pamoja na kuendelea kulinda na kuunga mkono maridhiano ya kisiasa ya Zanzibar.

Katika risala yao, iliyosomwa na Mratibu wa Wanawake wa kisiwa cha Pemba, Bi. Mkunga Hamad Sadala, kwa niaba ya Wana-ACT wa Mikoa ya Chake Chake na Mkoani, kisiwani humo kichama, wamebainisha azma waliyonayo katika kuondoa changamoto na kuepuka kukata tamaa, sambamba na dhamira ya kuungamkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, katika kuhamasisha maendeleo hapa visiwani.

Naye Mwenyekiti wa Wanawake wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Chake Chake kichama, Bi. Mpaji Abass Yussuf amewapongeza Wanachama wapya takriban 400 waliojiunga kupitia hafla hiyo, akisema ni ishara ya imara na azma yakuendeleza harakati za kufikia malengo muhimu ya kuipigania na kuijenga Zanzibar mpya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...