Katibu Mkuu wa   Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amewataka Watendaji wa Sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo kutoka Serikali ya Muungano ya Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kusimamia kikamilifu maazimio yanayofikiwa kwenye vikao vya pamoja vya ushirikiano kwenye sekta hizo ili kufikia malengo. 

Dkt. Abbasi ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga Kikao Kazi cha Ushirikiano Ngazi ya Wataalam wa Sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka Serikali ya Muungano ya Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) leo Oktoba 21, 2021 mkoani Dodoma katika Ukumbi wa Jengo la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Aidha, katika kikao hicho ambacho amekiongoza pamoja na Mwenyekiti Mwenza, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Khamisi Abdallah Saidi kutoka SMZ, Dkt. Abbasi amefafanua kuwa ili kufikia malengo yanayoazimiwa ni muhimu kuzingatia mambo makuu sita.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kijiwekea malengo yanayopimika, kujiwekea malengo makubwa, kutekeleza malengo hayo, kufanya kazi kwa pamoja kama timu mmoja, kuimarisha mawasiliano ya ndani na nje ya taasisi husika na kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika utendaji wa kila siku.  

“Kwa kweli hizi ndiyo siri kubwa za mafanikio ambazo zitatuvusha kwenye sekta zetu lakini kubwa kuliko zote ni kumtanguliza Mwenyezi Mungu baada ya kutekeleza mambo yote”. Amefafanua Dkt. Abbasi

Naye, Mwenyekiti Mwenza wa kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Khamisi Abdallah Saidi amemshukuru  Dkt. Abbasi kwa uratibu mzuri wa kikao hicho ambapo amefafanua kuwa vikao hivyo siyo tu vinasaidia uboreshaji wa sekta husika bali vinasaidia kuimarisha muungano baina ya pande mbili za Serikali.

Aidha, amesema vikao hivi vinasaidia kuimarisha  mahusiano wa kitaasisi ambapo amefafanua kwamba  sekta hizi zinagusa  maisha ya kila siku  ya wananchi.

Ameelekeza kila Afisa Dawati (Focal Person) kwenye kila sekta husika kwa upande wa Zanzibar kutoa mrejesho wa utekelezaji wa maazimio kila baada ya miezi mitatu badala ya kusubiri vikao vya ushirikiano vya pamoja baina ya pande mbili za Muungano.

Lengo la kikao hiki lilikuwa ni kujadili utekelezaji wa maazimio na maeneo ya ushirikiano kufuatia vikao vya ngazi ya Mawaziri vilivyofanyika Julai 2019 na Machi 2020 mkoani Dodoma.

Pia kikao hicho kimeshirikisha Idara ya Habari-MAELEZO.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...