Na. Mwandishiwetu ,Michuzi Tv

Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya amesema anatamani kuona kipindi cha kwanza cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anafungua migodi mipya mikubwa mitatu ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa. 

Aidha amewaelekeza wafanyabiashara wa madini nchini kuwa waadilifu na waaminifu katika biashara ya madini huku akiwataka wageni na wazawa kuacha tabia ya kulaghaiana kibiashara nje ya soko na badala yake wafanye biashara kwenye masoko ya madini chini ya usimamizi wa Afisa Madini.

Naibu Waziri Prof. Manya amebainisha hayo wakati wa mahojiano ya moja kwa moja  katika kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa na kituo cha runinga cha Azam.

    Ameeleza kuwa, uadilifu katika biashara ya madini utaendelea kulinda heshima ya nchi kwa kuuza madini halisi na kuwa na biashara za wazi zenye uaminifu ndani yake.

Prof. Manya amesema Wizara ya Madini kwa sasa inachangia Pato la Nchi kwa asilimia 6.7 hivyo kwa kufungua migodi mingine mipya kutatimiza lengo la Wizara la kuchangia kwa asilimia 10 ifikapo 2025.

“Tarajio langu ni kwamba, katika kipindi cha kwanza cha Rais Samia Suluhu Hassan kabla ya 2025 afungue migodi mingine mipya,  pale Sengerema-Nyanzaga wa Ore Corp, mradi wa kuchimba madini ya Graphite unaotekelezwa na kampuni ya Lindi Jumbo Limitedna mradi  wa Rare Earth uliopo katika Mkoa wa Songwe.

"Hii asilimia 3.4  iliyobaki 3.4  Wizara haitatushinda ili kufikisha asilimia 10 ya mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa,” amesema Manya.

Akizungumzia mipango ya Serikali katika kuiimarisha Sekta ya Madini, amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuyasimamia masoko yaliyoanzishwa maeneo mbalimbali nchini na kuhakikisha madini yanaongezwa thamani nchini kabla ya kusafirishwa nje ya nchi sambamba na kuimarisha migodi ya madini ya tanzanite ambayo inahitaji kutangazwa kikamilifu kutokana na upekee wake na kuwekewa mfumo wa kuyadhibiti.

Pia, suala la kusafisha madini nchini, Prof. Manya amesema, mpaka sasa Tanzania kuna mashine 417 za kung’arisha madini ya vito ambapo mashine 285 zipo Arusha, 95 zipo Dar es Salaam, 24 zipo Tunduru, huku 18 zikiwa Morogoro na Dodoma lengo ni kuhamasisha mashine ziongezeke ili ajira indelee kubaki nchini. 

Vile vile Prof. Manya amesema, Mwaka 2017 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ambapo moja ya kipengele kilichoongezwa ni pamoja na kampuni kubwa na za kati kutoa hisa huru ya asilimia 16 kwa serikali.

Amesema kuwa, kabla ya Marekebisho ya Sheria ya Mwaka 2017 muwekezaji yoyote alitakiwa kulipa Corporate Tax ya asilimia 30 na  tozo ya mrabaha wa asilimia 4, lakini katika muktadha wa sasa analipa mrabaha wa asilimia 6, ada ya ukaguzi asilimia 1 na ushuru wa huduma wa asilimia 0.3 ya Gloss, baada ya kufanya biashara yake pia anatakiwa kulipa Corporate Tax ya asilimia 30  na baadae kulipia asilimia 16 kama hisa huru .



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...