Na Samir Salum,Shinyanga
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamau Liberatus Sangu ameendelea kuwasisitiza vijana kutokubali kutumiwa kuvuruga amani ya nchi na badala yake watumie nguvu walizonazo kuujenga ufalme wa Mungu.
Ametoa rai hiyo leo Novemba 21,2021 wakati akiongoza Misa takatifu ya kufunga mwaka wa Kanisa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mama mwenye Huruma Ngokolo mjini Sinyanga ambayo imekwenda pamoja na kufunga kongamano la kijimbo la Vijana Wakatoliki wafanyakazi VIWAWA.
Amesema mara nyingi vijana wamekuwa wakitumiwa kufanikisha mipango ambayo imekuwa ikihatarisha hali ya amani katika mataifa mbalimbali jambo ambalo wanapaswa kulikataa na badala yake watumie nguvu na karama walizonazo katika kuujenga ufalme wa Mungu.
“Mara nyingi vijana wanatumiwa vibaya na watu ambao hawana nia njema kwa sababu wana nguvu sasa wanaweza kutumia nguvu zao vibaya,niwasihi vijana tumieni nguvu zenu katika kujenga ufalme wa mungu kwa kuwa chimbuko la haki,amani,upendo na umoja mahali kote duniani," amesema Askofu Sangu
Amewataka Watanzania kutochoka kumuomba Mungu ili aendelee kuimarisha misingi ya haki,amani,upendo na mshikamano hatua ambayo itasaidia kuliepusha taifa na hali ya migogoro na umwagaji damu ambao unatokea katika mataifa mengine kwa sababu tu ya ubinafsi wa watu wachache
Aidha amewapongeza Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA)Jimbo la Shinyanga kwa namna ambavyo wamejitoa katika kulilea shirika jipya la watawa la kijimbo la Mtakatifu Bikra Maria Mama mwenye Huruma ambalo limeanzishwa miaka michache iliyopita.
Amesema WAWATA wamefanya kazi kubwa katika kulilea na kulitunza shirika hilo hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto zilizopo.
“Nichukue Nafasi hii kuwashukuru sana WAWATA wamekuwa mstari wa mbele sana katika mwaka wote huu na miaka iliyopita katika kulitiunza na kulilea shirika letu la Bikira Maria Mama wa Huruma,"amesema Askofu Sangu
Wakati huohuo Askofu Sangu amewaongoza waamini kusali kuliombea taifa ili lipate mvua za kutosha kutokana na hali ya hewa kwa mwaka huu kutokuwa ya kuridhisha ikiwa ni mwendelezo wa kuunga mkono mwito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alioutoa kwa viongozi wa dini hivi karibuni jijini Mwanza.
Kupitia Misa ya leo ambapo pia kanisa linaadhimisha Jumapili ya Kristo Mfalme,askofu Sangu pamoja na mambo mengine amewabatiza watoto wadogo wapatao 88.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...