Na Mwandishi Wetu
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo Othman Masoud Othman ameeleza dhima aliyonayo katika kuutumikia umma wa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, ili kufanikisha matarajio yao makubwa ya kujikwamua kimaisha na kujiletea maendeleo.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo Kojani Mjini wakati akizungumza na Wazee, Wanachama, Wafuasi wa ACT-Wazalendo na Wakaazi wa Kisiwa hicho, katika ziara yake Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema anaelewa tofauti iliyopo kati yake na Mtangulizi wa Nafasi hiyo, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, bali atahakikisha anatekeleza dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wote wa Visiwa vya Unguja na Pemba, na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza kuhusu upekee wa Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, Mheshimiwa Othman ametaja Kipaji katika kutetea haki, vita dhidi ya dhulma na uzalendo wa kweli, na kwamba atakuwa tayari kuyaendeleza hayo kwaajili ya maslahi ya wananchi wote.
Othman amesisitiza umuhimu wa amani, utulivu, umoja na mshikamano katika jamii ili kuandaa mazingira bora yatakayotoa fursa kwa Serikali kutekeleza mipango yake kwa ufanisi na hatimaye wananchi kupata maendeleo.
Akimkaribisha Mgeni rasmi, Naibu katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar ambaye pia ni Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto hapa visiwani Nassor Ahmed Mazrui amesema Serikali inao wajibu wa kukabiliana na kero za wananchi, huku akiahidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto thakili za kisiwa hicho, zikiwemo upungufu wa huduma za matibabu na ukosefu wa madaktari.
Nao Wazee wa Kojani ambao wamemkabidhi rasmi Mheshimiwa Othman kisiwa hicho, wameeleza matumaini waliyonayo na kwamba wamempokea kiongozi huyo kwa moyo wote, wakitaraji utekelezaji wa dhamira na heshima ya dhati kwao kama ilivyokuwa kwa Maalim Seif zama za uhai wake.
Wakibainisha changamoto zinazowakabili, Mzee Faki Mwinyimkuu Hassan, Bakari Juma Maua, Mjaka Hamad Mjaka na Bi Shine Mfaki, wametaka kuelewa hatua za utekelezaji wa dhati wa makubaliano kati ya Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dokta Hussein Ali Mwinyi, katika kufanikisha maridhiano ya kweli ya kisiasa hapa visiwani.
Katika ziara yake ya kwanza kisiwani humo iliyopokelewa kwa mapokezi makubwa na Wakaazi wa Kojani, vikundi vya burudani na kuwakagua wagonjwa, Mheshimiwa Othman aliongozana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, Katibu wa Oganaizesheni wa ACT-Wazalendo Ndugu Omar Ali Shehe, Wajumbe wa Kamati kuu, Wawakilishi, Wabunge, na viongozi mbali mbali wa Chama hicho.
Wakati huo huo Mhe.Othman ameshiriki katika shughuli ya maziko ya Bwana Ali Kombo Hassan, ambayo yamefanyika jioni ya leo katika kijiji cha Kambini Mchanga mdogo, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...