Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imejipanga kuongeza shehena ya mizigo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inayopita Bandari ya Dar es Salaam kutoka tani milioni 1.9 za sasa hadi kufikia tani milioni 3 kwa mwaka katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Akizungumza na wafanyabiashara wa DRC, wanaosafirisha mizigo yao kupitia Bandari ya Dar es Salaam katika kikao kilichofanyika mjini Lubumbashi chenye lengo la kusikiliza changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Eric Hamissi amesema wamejipanga kutimiza lengo hilo katika kipindi cha miaka miwili kutoka sasa.
Hamissi amesema kwamba TPA imeanzisha kampeni maalumu za kimasoko ili kutanua wigo na kuvutia wafanyabiashara wengi zaidi kutumia Bandari ya Dar es Salaam.
Amesema kwamba kumekuwa na ongezeko la shehena ya mizigo ya DRC inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam kwa wastani wa asilimia 57, kutoka tani 1.1 milioni kwa mwaka 2016/17 hadi kufikia tani milioni 1.9 kwa mwaka 2020/21
"Ongezeko hili limetokana na maboresho ya miundombinu yanayoendelea, kuongeza vifaa, kina cha magati na kampeni za kimasoko pamoja na kuboresha huduma zetu kwa wateja". Aliongeza kwamba kama bandari, tunazidi kuongeza ufanishi ili kuhudumia shehena nyingi zaidi ambayo itaongeza mapato kwa TPA na nchi kwa ujumla.
Katika kikao hicho ambacho kiliandaliwa na TPA ili kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wasafirishaji wa DRC, kilihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Abdi Mkeyenge, Balozi wa Tanzania nchini DRC, Gavana wa Jimbo la Katanga, Mbunge wa Kalambo na wadau wengine wa Bandari wakiwemo, TRA, Dar es Salaam Corridor, TAFFA ,TAZARA na TASAA kilifanyika mjini Lubumbashi kwa mafanikio makubwa.
Mkurugenzi Mkuu TPA Eric Hamissi( kulia) akimkabidhi zawadi Gavana wa Jimbo la Katanga Mjini Lubumbashi nchini Congo DRC Jacques Kyabula Kakwe( kushoto).Matukio mbalimbali katika picha wakati wa kikao cha wadau wa Bandari ya Dar es Salaam wa nchini Congo DRC ambao wamekutana katika Mji wa Lubumbashi kama moja ya mkakati wa kupanua wigo wa biashara kati ya Tanzania na Congo DRC kupitia sekta ya bandari
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...