* Latoa vifaa vya usafi vyenye thamani ya shilingi milioni 10
KATIKA kuadhimisha siku ya choo duniani ambayo hufanyika kila tarehe 19 Novemba duniani kote, shirika la WaterAid Tanzania limeungana na taasisi nyingine kuadhimisha siku hii katika hospitali ya mama na mtoto Chanika kwa kufanya usafi vyooni na kutoa msaada wa vifaa vya usafi huku maadhimisho hayo yakibebwa na kauli mbiu ya "Kipe Hadhi Choo Chako" yaani 'Valuing Toilets.'
Katika maadhimisho hayo WaterAid imetoa vifaa vya usafi kwenye hospitali ya mama na mtoto Chanika na kituo cha afya cha Buguruni. Pia imetoa vifaa vya usafi kwa kikundi cha Hekima Kwetu kupitia kampeni yao ya “Choo safi, Hadhi Yangu”.
Vifaa vya usafi vilivyotolewa ni pamoja na mafagio, sabuni, mikokoteni, mabuti, majaketi ang’avu, glavu ngumu, mafagio pamoja na vifaa vingine vyenye jumla ya gharama ya shilingi milioni 10,000,000/=.Kama sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo.
Katika maadhimisho hayo pia umoja wa cha Hekima Kwetu kimeshirikiana na na ofisi ya halmashauri ya jiji ambapo kwa pamoja walifanya usafi katika Hospitali ya mama na mtoto Chanika na Kituo cha afya Buguruni pamoja na shule za msingi 8 zilizopo katika wilaya ya Ilala.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi katika maadhimisho ya siku hiyo, Mkurugenzi Mkaazi wa shirika la Wateraid Bi Anna Tenga Mzinga aliipongeza Serikali kwa juhudi inazochukua katika kuhakikisha jamii inakuwa na vyoo safi na salama.
“Napenda kuipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Tanzania kwa juhudi kubwa ambayo imefanya mpaka hivi sasa ambapo kwa mujibu ya ripoti ya Wizara ya Maji, kwa mwaka 2020 mafanikio yanaonyesha asilimia 66 ya kaya Tanzania wana vyoo bora majumbani ukilinganisha na asilimia 31 mwaka 2016.'' Amesema.
Amesema kwa upande wa masuala ya vyoo, WaterAid Tanzania imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa Serikalini na mashirika yasiyo yaki serikali ikiwemo kutoa mafunzo namna ya kujenga vyoo bora na stahimilivu pamoja na ujenzi kwenye baadhi ya maeneo mbalimbali nchini na kutoa mafunzo ya afya na usalama pamoja na kutoa vifaa vya usalama na usafi kwa wafanyakazi wa usafi wa vyoo sambamba na kushiriki kikamilifu kwenye kampeni za kitaifa ikiwemo Nyumba ni Choo.
Bi Anna Tenga Mzinga alieleza kwamba pamoja na mafanikio hayo, bado kuna uhitaji wa kuendelea kuhamasisha ili ifikapo 2030, kila nyumba iwe na choo bora na kuongeza kwamba kauli mbiu ya ya mwaka huu inaangazia ukweli kwamba Serikali, wadau wa maendeleo na watekelezaji kuna jukumu la kutoa kipaumbele na kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya vyoo ikiwemo mifumo bora ya maji na vifaa vya usafi wa vyoo.
“Suala la vyoo linamgusa kila mmoja wetu bila kujali hadhi na hali. Watoa maamuzi katika ngazi mbalimbali za Serikali, watekelezaji na wadau, tunaomba sote tufanikishe haya matatu; kwanza – vyoo bora, pili uwepo wa maji chooni na tatu vifaa vya kunawia mikono baada ya kutoka chooni kwa ajili ya usafi binafsi. Kama shirika tumeona leo tuwape vifaa vya kufanyia wahudumu wa usafi kwenye vituo hivi vya afya pamoja na kikundi hiki kiimarishe usafi kwenye vyoo sehemu za Taasisi huku tukitoa wito kwa Serikali, Wadau wa maendeleo kuongeza bajeti kwenye masuala ya usafi wa mazingira ili kuepukana na milipuko ya magonjwa yanasyosababishwa na uchafu”
Bi Anna Tenga Mzinga alieleza kwa wanawake na wasichana, vyoo bora vya nyumbani, shuleni na vituo vya kutolea huduma za afya huwasaidia kutimiza uwezo wao na kutekeleza wajibu wao kikamilifu katika jamii, hasa wakati wa hedhi na ujauzito.
''Mfano kukiwa na vyoo bora vyenye mifumo bora ya maji shuleni, wasichana hawatabaki nyumbani wanapokuwa kwenye hedhi kama ambavyo ripoti ya Hali ya Afya ya Hedhi na usafi miongoni mwa wasichana wa Shule nchini Tanzania inavyoeleza.
WaterAidWaterAid Tanzania ni Shirika la kimataifa lenye dira ya kuhakikisha kuwa watu wote ulimwenguni wanapata maji ya uhakika, vyoo bora na huduma za usafi zilizoboreshwa ifikapo mwaka 2030. WaterAid inafanya kazi katika nchi 34, ambapo nchi 18 zipo barani Afrika. Nchini Tanzania, Shirika la Wateraid lilianza kazi 1983 na kufanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya Maji, Vyoo na Usafi binafsi katika zaidi ya mikoa 11. Aidha shirika limeshirikiana na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo na kuwafikia wananchi zaidi ya milioni nane wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa miji pamoja na vijijini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...