*WaterAid yatoa vifaa vya usafi katika maadhimisho ya siku ya choo duniani
MATUMIZI bora na salama ya vyoo kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam yameimarika kutoka asilimia 70 hadi kufikia asilimia 95.4 huku uwepo wa sehemu maalum ya unawaji ukiimarika na kufikia asilimia 67 kutoka asilimia 8 hali iliyopelekea kupungua kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Hayo yameelezwa na Afisa Afya wa jiji la Dar es Salaam Reginald Mlay wakati wa maadhimisho ya siku ya choo duniani yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwa kauli mbiu ya 'Kipe Hadhi Choo Chako' hafla iliyokwenda sambamba na shirika la WaterAid kufanya usafi wa vyoo na kugawa vifaa vya usafi katika zahanati ya Chanika, kituo cha afya Buguruni na kikundi cha 'Hekima Kwetu' kupitia kampeni yao ya 'Choo Safi, Hadhi Yangu'
Mlay amesema wamekuwa wakihamasisha wananchi kujenga vyoo bora na salama katika matumizi na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika uhamasishaji wa ujenzi waa vyoo bora pamoja na kufundisha mafundi sanifu 26 kutoka kila Kata ambao wamekuwa msaada katika ujenzi wa vyoo vya Umma na shule.
Amesema, katika kusaidia kila Kaya inakuwa na vyoo salama wametoa vyoo maalum (smart toilets) kwa Kaya maskini 729 na shule 42 ambazo zimepatiwa vyoo 615 kwa ufadhili wa kampuni SATO.
Kuhusiana na uhamasishaji wa ujenzi wa vyoo bora na salama Mlay amesema wamekuwa wakikumbana na changamoto maji katika shule pamoja na changamoto ya usafiri katika kufuatilia na kusimamia ujenzi wa vyoo bora na salama.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng'wilabuzu Ludigija amemtaka Afisa Afya wa jiji hilo na timu yake kumalizia asilimia nne zilizobaki ili kufikia asilimia 100 ya matumizi ya vyoo bora na kuhakikisha kunakuwa na huduma za choo katika stendi za mabasi na katika mikusanyiko.
Ng'wilabuzu amesema elimu zaidi ya unawaji mikono na utumiaji sahihi wa vyoo iendelee kutolewa hasa kwa wanaohamia katika makazi mapya bila kuwa na huduma ya choo.
Pia amelishukuru shirika la WaterAid kwa msaada wa vifaa hivyo pamoja na kuwa wadau wakubwa wanaoshirikiana na Serikali katika kutoa elimu kwa Umma kuhusiana na matumizi sahihi ya vyoo.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Chanika 'Nguvukazi' Dr. Paschal Nkii ameeleza changamoto kubwa ya maji ya chumvi ambayo hugharimu pesa ya nyingi za ukarabati wa vifaa vya vyoo ambavyo huathiriwa na maji hayo jambo ambalo Ngw'ilabuzu alihaidi kulichukulia hatua za haraka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...