WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi,
Prof. Makame Mbarawa, amesema kuwa Serikali imedhamiria kujenga barabara
inayoanzia Sale hadi Ngarasero (km 50) kwa kiwango cha lami ili kufungua uchumi
wa Ngorongoro, kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji na kukuza utalii.
Aidha, ameiagiza Wakala wa
Barabara (TANROADS), kuanza usanifu wa sehemu ya barabara ya Wasso – Loliondo
(km 10) ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
Prof. Mbarawa amesema hayo wilayani
Ngorongoro mkoani Arusha, wakati akikagua mradi wa barabara ya Mto wa Mbu –
Loliondo (km 217) sehemu ya Wasso – Sale (km 49), inayojengwa kwa kiwango cha
lami na kumtaka mkandarasi China Wu Yi kukamilisha barabara hiyo mapema
mwanzoni mwa mwaka 2022.
“Serikali kwa kujua umuhimu wa
eneo hili imeamua kujenga barabara hii kwa awamu, tunamaliza kilometa 49 sasa na
kuanza na kilometa 50 nyingine ili wananchi waweze kusafiri kwa kutumia
barabara ya lami”, amefafanua Waziri Mbarawa.
Aidha amewataka wananchi wa maeneo
hayo kuitunza na kuilinda barabara hiyo kwa kutopitisha ovyo mifugo katika
barabara pamoja na kuharibu alama za barabara ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
“Ninawaombe wananchi wa hapa
ambao ni wafugaji wazuri muilinde hii barabara na mifugo ipite katika maeneo
maalum yatayotengwa kupitisha mifugo”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Akitoa taarifa ya mradi, Mhandisi
Mshauri wa mradi kutoka TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU), Mhandisi
Mbaraka Shafi, ameeleza kuwa mradi umefikia asilimia 97 na unaratajiwa
kukamilika ifikapo mwezi Aprili, 2022.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Ngorongoro, Raymond Mangwala, amemueleza Waziri huyo changamoto wanazozipata
katika utekelezaji wa miradi ikiwemo wanapotangaza zabuni mara nyingi watu
hawafiki eneo hilo kutokana na jiografia ngumu ya wilaya hiyo.
“Kupata mkandarasi huku ni ngumu
hivyo kwa kuwa mkandarasi huyu tayari ana vifaa vyote na anaujua uzoefu wa huku
angepewa barabara zingine ili tuweze kuufungua kwa haraka mkoa wa Arusha na
Mara”, amesema Mangwala.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa ameipongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mkoa wa Arusha kwa usimamizi na ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na kuwataka wakamilishe jengo hilo mapema iwezekanavyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...