Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
SERIKALI
kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetenga
shilingi bilioni 7.3 kwa ajili ya kufungua barabara za Halmashauri ya
Wilaya ya Iramba mkoani Singida ikiwa ni utekelezaji wa kauli mbiu yake
ijulikanayo kama ‘Tunakufungulia barabara kufika kusikofikika’.
Akiwa
katika ziara ya kikazi wilayani humo,Waziri wa Nchi Ofisi ya Raia
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Ummy
Mwalimu amesema azma ya Serikali ni kufungua barabara za vijijini ili
wananchi waweza kufanya kazi zao bila kikwazo cha usafiri.
Akikagua
barabara ya Shelui - Tintigulu inayojengwa kwa urefu wa kilomita saba,
Waziri ameelekeza barabara hiyo ijengwe kwa ubora unaotakiwa ili iweze
kudumu na kuwasaidia wananchi wa Shelui katika shughuli zao za kila
siku.
"Lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia
Suluhu Hassan ni kuwafungulia wananchi wa vijijini barabara ili isiwe
kikwazo tena katika shughuli zao na hapa nimeona baada ya barabara hii
kukamilika inakwenda kufungua na kurahisisha mawasiliano ya kata tatu na
vijiji sita,"amesema.
Pia Waziri Ummy alimuelekeza Meneja wa
TARURA Wilaya ya Shelui, Mhandisi Evance Kibona kuhakikisha kuwa
wanafanya usanifu wa Daraja la Nshoka linalounganisha kata za Shelui -
Tintigulu ili barabara hiyo inayojengwa iweze kuleta manufaa zaidi kwa
wananchi wa maeneo hayo.
"Nimekagua ujenzi wa barabara, umeanza
lakini nimeona kuna mto Nshoka ambao unatakiwa kujengewa daraja ili
barabara hii inayojengwa iweze kuleta manufaa, vinginevyo bado watakuwa
wanapata usumbufu wakati wa mvua nataka tumalize kabisa changamoto hii.
"Mto
huu ni mkubwa na hakuna daraja sasa wakati wa mvua wananchi hawawezi
kupita hapa hivyo ni vyema hapa pakajengwa daraja ili barabara hii iwe
na tija stahiki, hivyo wahandisi anzeni kufanya usanifu na muingize
kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 tuweke ujenzi wa daraja hili
kwenye bajeti yetu.
Akizungumza wakati wa ukaguzo wa barabara
hiyo ya Shelui-Tintigulu Meneja wa TARURA Wilaya ya Iramba, Mhandisi
Evance Kibona amesema, ujenzi wa barabara hiyo umeanza Desemba 11 na
utakamilika Juni,2022.
Pia ameeleza kuwa,barabara hiyo
itakayokuwa na urefu wa kilomita saba itagharimu shilingi milioni 524 na
inajengwa kwa kiwango cha lami.
Barabara hii inajengwa kwa fedha
kutoka katika tozo na ikikamilika itaunganisha kata tatu na vijiji sita
vyenye wakazi zaidi ya 14,000.
Kwa mwaka wa fedha 2020/21 bajeti
ya miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Iramba ilikuwa milioni 860
na katika mwaka wa fedha 2021/22 bajeti hiyo imeongezwa mpaka kufikia
shilingi bilioni 7.3
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...