NA BALTAZAR MASHAKA, KAHAMA

FAMILIA ya Mpira wa Miguu imepata pigo kufuatia kifo cha Katibu wa Bodi ya Kahama Sports Academy na Katibu Mkuu wa klabu ya Kahama United,iliyowahi kushiriki ligi kuu, Shaaban Nguno.

Marehemu huyo aliyewahi kuwa Katibu wa Tawi la Simba Mjini Kahama, alizikwa juzi kwenye makuburi ya Nyihogo wilayani Kahama, ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo, Festo Kiswaga, aliwaongoza maelfu ya waombolezaji.

Akitoa salamu za pole kwa familia, waombolezaji na wakazi wa Manispaa ya Kahama, Kiswaga alimwelezea nguli huyo wa michezo alimfahamu kupitia kwa Khamis Mgeja katika harakati na ushirikiano wa kuendeleza michezo wilayani humo.

"Marehemu Nguno alikuwa na ushirikiano na mstari wa mbele wa kuendeleza michezo kwenye wilaya yetu, nitoe pole kwa wananchi na wadau wa michezo,wilaya, mkoa na taifa kwa kuondokewa na mdau mkubwa wa maendeleo ya sekta ya michezo na tuendelee kuyaenzi mazuri aliyotuachia," alisema Kiswaga.

Kwa upande wake Sheikhe wa Wilaya ya Kahama, Sheikhe Omar Damka, alisema kuwa marehemu Nguno aliishi vizuri na jamii, kielelezo ni waombolezaji waliojitokeza kumsitiri kwenye safari yake ya ahera.
Aliwaomba wananchi na waombolezaji bila kujali itikadi za dini zao waendelee kushirikiana kama jamii inayoishi pamoja kama alivyoishi Nguno.

"Hata Mtume Muhhamad S.A.W anatuasa 'shirikianeni na watu wote' hajasema ushirikiano uwe kwa waislamu pekee.Huo ndiyo wosia wa mtume wetu na marehemu Nguno aliishi maisha hayo ya ushirikiano na jamii," alisema Sheikhe Damka .

Aliwaasa waombolezaji kushirikiana, kulinda umoja na mshikamano katika maisha yao ya kila siku ya hapa duniani.

Naye Mwenyekiti Bodi ya Wadhamini ya Kahama United Sports Academy, Khamis Mgeja,akitoa neno ka shukurani kwa niaba ya familia na wadau wa michezo alimwelezea Nguno kuwa alikuwa mwana michezo wa mfano.


"Hata kuanzishwa kwa Kahama Acadeny alikuwa mmoja wa waasisi hadi umauti unamkuta na alikuwa Katibu wa Bodi ya Wadhamini ya kituo hicho cha kukuza vipaji,"alisema

Mgeja alizungumzia marehemu Nguno katika uhai wake na maisha ya soka alikuwa mlinda mlangomahiri na alichezea klabu ya soka ya Mamlaka ya Pamba Shinyanga na aliwahi kuwa katibu msaidizi wa klabu yaToto Africa ya Mwanza.

Pia alieleza kuwa alishirikiana na Nguno kuendesha Kahama United akiwa Katibu Mkuu wakati ikicheza ligi kuu,alikuwa na moyo kujitolea hasa katika masuala ya michezo, alikuwa mstari wa mbele kupanga mikakati na mwenye mipango mizuri ya kuwaendeleza vijana kisoka.

Kwa mujibu Mgeja marehemu Nguno aliwahi kuwa Katibu wa Simba, tawi la Kahama Mjini,hivyo kwa hakika familia ya michezo imeondokewa na mdau muhimu na mchango wake bado ulikuwa ukihitajika hasa mipango ya kuendeleza vipaji vya vijana kisoka.

"Kwa vile ni mapenzi ya Mungu tunashukuru kwa mwenzetu kutangulia mbele ya haki, nitumie fursa hii kuwashukuru watu wote wa rika mbalimbali walioshiriki maziko ya Nguno wakiongozwana Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Ushirika,Charles Gishuli na waandishi wa habari za michezo," alisema Mgeja na kuomba mazuri aliyoyafanya yaenziwe.

Marehemu Shaaban Nguno,ameacha watoto sita,wa kiume wawili na wa kike 4, alizaliwa Februari 14, 1954 na kufariki Disemba 17,mwaka huu na kuzikwa juzi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...