Na Amiri Kilagalila,Njombe
Wananchi wa kijiji cha Kilenzi kata ya Uwemba halmashauri ya mji wa Njombe wamesema hulazimika kugoma kuhudhuria katika mikutano inayoendelea katika maeneo yao kutokana kuahidiwa kutatuliwa changamoto ya upatikanaji wa maji zaidi ya miaka 30 sasa bila mafanikio.
Hata hivyo wamesema licha ya ahadi ambazo hutolewa na viongozi mbali mbali katika kijiji chao hususani wakati wa kampeni lakini tatizo la ukosefu wa maji limeshindwa kutatuliwa hali inayowafanya kuto kuona umuhimu wa kudhuria kwenye mikutano inayoitishwa kijijini kwao.
Imelda Kawogo na Olaph Mdetele ni miongoni mwa wananchi wa kijiji cha Kilenzi,mbele ya mkutano wao na wataalamu kutoka wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Njombe uliofanyika katika ofisi za kijiji hicho wanasema kufika kwa wataalamu hawa na kutoa ufafanuzi juu ya kutatua changamoto hiyo mapema mwakani kumeleta matumaini makubwa kwao.
“Wananchi wamesema hivi hawapo tayari kumsikiliza mwenyekiti au kusogea kwenye mikutano kama hawatapewa maji”alisema Imelda Kawogo
Olaph amesema “Kama kweli maji yatakuja kwasababu swala la maji huwa linaongelewa kila siku hapa tunaona kama ni ndoto kwasababu kila mwaka linaongelewa hivi hivi lakini pale tutakaposkia twende kwenye maendeleo nitashukuru sana na mimi nitapiga makofi zaidi nitakapoona tayari kitu kinaonekana”
Kwa upande wake mtaalamu wa maji kutoka RUWASA mhandisi Bakari Kitogota amewatoa hofu wananchi wa kijiji hicho kwa kuwa tayari kibali cha ujenzi wa mradi wa maji wa kijiji hicho kupitia chanzo kilichopo katika mpaka wa kijiji cha Njomlole na Luponde kimekwishatoka na mradi unatarajiwa kuanza mapema mwishoni mwa mwezi wa kwanza mwaka 2022.
“Mradi wenu unaanza na kibali tumeshapata kwa hiyo mwishoni mwa mwezi wa kwanza yaanai mwanzoni mwa mwezi wa pili tutafanya kazi hapa Kilenzi na tunajua chanzo cha hapa kinatokea Kilenzi ndio maana tumeona tuje tuongee ili muondokane na dukuduku lenu”alismea Kitogota
Naye diwani wa kata ya Uwemba bwana Jactan Mtewele ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwaona wananchi wa kijiji hicho kwa kuwa wamekuwa na uvumilivu mkuwa licha ya kukosa maji.
“Tunashukuru sana leo wamekuja sasa kutupa majibu sahihi kwamba tayari kibali kimekwishakupatikana na yote haya inaonyesha ni jinsi gani ambavyo tuna Rais shupavu kwa kupamabana na kuweza kutuletea pesa katika kijiji chetu”alisema Jactan Mtewele
Baadhi ya wananchi wa Kilenzi wakitoka katika ofisi ya kijiji hicho baada ya mkutano baina ya wananchi na wataalamu kutoka RUWASA uliofanyika katika kijiji hicho ili kuzungumzia changamoto ya maji.Diwani wa kata ya Uwemba bwana Jactan mtewele akizungumza baada ya kuridhishwa na taarifa ya wataalamu kutoka RUWASA juu ya kuanza kwa mradi wa maji wa kijiji cha Kilenzi.
Mhandisi Bakari Kitogota kutoka wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilayani Njombe akiwatoa hofu wananchi wa kijiji cha Kilenzi na kuahidi kuanza ujenzi wa mradi huo ili kutatua changamoto ya maji.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...