Kazi za ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami katika Kiwanja cha Ndege cha Musoma zikiendelea, mkoani Mara.
PICHA NA WUU
IMEELEZWA kuwa pindi Ujenzi wa
Kiwanja cha Ndege cha Musoma utakapokamilika utafungua usafiri wa anga kwa mkoa
wa Mara na kuwa kiunganishi kikubwa na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa.
Hayo yamesemwa mkoani Mara na Waziri
wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati akikagua ujenzi wa barabara
ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilometa 1.75 ambapo
utaruhusu ndege za Q400 Bombadier kutua kwa urahisi kiwanjani hapo.
Prof. Mbarawa amesema ameridhishwa
na maendeleo ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma unaogharimu kiasi cha
shilingi bilioni 35.047 na mkandarasi anayetelekeza mradi huo ni Beijing
Construction Company Limited ambapo kazi zinaendelea kwa kasi.
“Kiwanja cha Ndege cha Musoma
kitakapokamilika kitafungua anga kwa kiasi kikubwa na kukuza uchumi wa mkoa wa
Mara na mikoa jirani”, amesema Prof. Mbarawa.
Kuhusu suala la fidia, Waziri
Mbarawa amesema Serikali imekwisha lipa fidia kiasi cha shilingi Bilioni 3.955
kwa wananchi waliopisha ujenzi huo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja
wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma, Bw. Frank Msoffe amesema kuwa ujenzi wa
kiwanja hicho utakapokamilika utatoka katika daraja la 2C na kwenda 3C na
kuruhusu kupokea ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 70 hadi 80.
Naye Meneja wa Wakala wa
Barabara (TANROADS), mkoa wa Mara Mhandisi Vedastus Maribe, ameeleza kuwa mradi
huo unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba 2022 na unahusisha barabara ya kuruka
na kutua ndege, barabara ya maegesho ya ndege, jengo la kuongezea ndege na
jengo la zima moto.
Katika hatua nyingine, Waziri
Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Sanzate – Nata (km 40) kwa kiwango
cha lami inayojengwa kwa gharama ya zaidi shilingi bilioni 39 na kumuagiza
mkandarasi China Railway Seventh Group kuongeza kasi ya ujenzi huo na
kukamamilisha kwa muda uliopangwa wa miezi 24.
Prof. Mbarawa amesema kiasi cha
shilingi Bilioni 1.047 zitalipwa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi 291
waliothiriwa na ujenzi wa barabara hiyo.
Barabara hiyo ni sehemu ya
barabara kutoka Musoma – Arusha kupitia Serengeti Mto wa Mbu ambayo ni kiungo
muhimu kati ya Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini na nchi jirani ya
Kenya.
Waziri Mbarawa yupo mkoani Mara kwa ziara ya siku mbili ya kukagua utekelezaji wa miradi inayoendelea kutekelezwa na Wizara yake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...