Adeladius Makwega,Dodoma.
Siku ya jana nilisafiri kutokea Lushoto kuja Dodoma na kwa bahati nzuri nilipata usafiri kwani tiketi nilikata mapema siku tatu kabla ya safari yangu hiyo kuepukana na changamoto ya usafiri katika siku za mwisho wa mwaka.
Kulingana na tiketi yangu nilipaswa kukaa kiti namba 13 lakini kwa kuwa basi hilo lilipoanza safari Lushoto kuna abiria waliopanda ambao walikuwa wakishuka Korogwe kwa hiyo pahala nilipotakiwa kukaa alikaa abiria mmoja ambaye binafsi niliona siyo busara, atakaposhuka nitakaa nafasi hiyo isitoshe viti vingi vilikuwa wazi.
Tulipoanza safari kutokea Lushoto Mjini nilidhani basi hilo lipo tupu lakini tulipofika Korogwe abiria waliingia wengi na kusababisha kweli basi hilo kujaa hapo hapo na mimi kuhamia katika kiti changu.Safari ilianza na kuondoka Korogwe vizuri kwa mwendo wa kiistarabu wa dereva wetu wa siku hii.
Muundo wa siti za basi hili ulikuwa ni siti mbili mbli kila upande na katikati ni njia ya kupita, kwenye siti yangu nilikaa mimi na mama mmoja na upande wa kushoto kwangu alikuwepo mama mmoja mtu mzima na kijana mmoja.
Kumbuka mimi nimeanzia safari Lushoto bali huyu mama amepanda Korogwe na alipopanda tu nilibaini kuwa ni mama makini kwanza alikuwa amevalia barakoa vizuri sana na huku akiwa na kipukutishi na kila mara alikuwa akijimiminia mikononi angalau awe salama. Alipokuwa akijimiminia kipukutishi hicho kilisababisha na mimi kupiga chafya sana sana ambapo kabla ya hapo sikuwahi kupiga chafya yoyote kwa miaka mingi.
Katika siti hizi nne hakuna mtu mwingine aliyevali barakoa zaidi ya yeye. Tukiendelea na safari nilipomuangalia vizuri nilibaini kwa umri wake alikuwa ni bado mdogo bali alikuwa amevalia baibui vizuri sana na kutokana na joto la safari alikuwa sasa anajifungua na mie nilikuwa namkodolea kwa wizi angalau niweza kumuona vizuri. Basi lilipokuwa linazidi kwenda nilibaini kuwa mama huyu alikuwa ni mweupe na alisuka twende kilioni.
Kwa kuwa safari za mwisho wa mwaka usafiri unakuwa mgumu, basi hili lilipata abiria zaidi kwa hiyo baadhi ya abiria walikaa katikati huku wakipatiwa ndoo/vigoda vya kuketi. Kwa sasa katika mstari ule wa kushoto na kulia abiria wawili wawili abiria mmoja wa kati kwa hiyo kulikuwa na abiria watano.
Huyu mama jirani yangu yeye tangu alipokuwa amepanda Korogwe alikuwa na begi mgongoni alipokaa akalipakata juu ya miguu yake huku akipata nalo tabu kweli kweli, tangu wakati anaingia Korogwe alikuwa na nafasi ya kuweka katika sehemu ya kuweka mizigo lakini hakufanya hivyo, aliendelea kulibeba safari yote.
Basi liliendelea na sasa lilifika Msata ambapo kuna mizani, lilisimama na abiria kushuka na kwenda kujisaidia na kurudi kuendelea na safari yetu.
Dereva wetu aliendelea kuendesha vizuri na sasa tukawa tunakaribia kufika Morogoro, huku mimi nipo na abiria mwezangu ambaye kwa hakika alikuwa anaheshimu masuala ya afya haswa haswa Korona lakini ana mzigo ameubeba na mzigo huo unaonekana ni mzito na unamchosha lakini nitawezaje kumwambi auweke chini?
Pengine ameweka fedha zake zikiibiwa itakuwaje? Pengine kaambiwa na mganga wa kienyeji hilo begi unaposafiri haupaswi kulishusha, likae mapajani mwako mwanzo mwisho. Maana kila mtu na imani yake. Mimi niliendelea kuwa kimya na kumtazama ndugu yangu huyu anavyoteseka.
Tulifika Msamvu na abiria kadhaa walishuka nadhani hao walikuwa wakielekea mikoa ya Mbeya na Ruvuma, wakati sisi tunaelekea Dodoma. Mara baada ya abiria hao kushuka, basi lilipitia hoteli moja tulikula chakula na kuendelea na safari. Mpaka muda huo mimi, mama mpakata mabegi na wale ndugu wezangu wa kiti cha mkono wa kushoto nadhani wote tulikuwa abiria wa Dodoma kwa hiyo hakuna aliyeshuka Msamvu.
Safari iliendelea hadi Gairo, huku ndugu yetu mama mpakata begi akiwa amechoka kweli kweli, sasa mama wa upande wa kushoto katika siti ya kushoto alimueleza, sasa wewe huoni unateseka na begi ukiwa umelipakata tangu Korogwe hadi huku kana kwamba umebeba mtoto? Kweli unadhani utafika salama Dodoma? Na hata ukifika salama unaweza kupata madhara ya kiafya.
Kweli eh? Aliuliza huyu mama mpakata mabegi mapajani. Mama alimjibu kweli.
”Unajua humu nimeweka kompyuta nilidhani inaweza kuharibika.”
Mama huyu alimwambia sasa kompyuta na hilo paja lako kipi cha thamani kwako? Hiyo kompyuta ikifa utanunua nyingine lakini huo mfupa wa paja ukivunjika?
Basi mama huyu mpakata begi alisimama na kulichukua begi lake na kuliweka chini ya kiti nayeye kukaa kwa amani tangu Gairo hadi Dodoma na kufika Dodoma Salama salimini.
Hoja ya leo ni moja tu, katika maisha wapo watu ambao wanakuwa na mizigo wameibeba wakidhani kuwa ina thamani kubwa kumbe haina lolote bali imekuwa ikiwaumiza na kuwatesa pengine bila ya wao kufahamu hilo. Wapo watu wanaoona kuwa hapa mwenzetu ameelemewa na huo mzigo lakini hawakwambii kwa hofu nyingi tu, ah pengine mganga wake kamwambia alishikilie/pengine kuna fedha ndani yake, ngoja mimi nikae kimya tu. Kumbe mwezenu anaumia. Kuna madhara ya moja kwa moja wakati huo huo lakini yapo madhara ya baada ya kumaliza safari.
Kwa bahati nzuri mama huyu alipoambiwa alikuwa muelewa kwa haraka na mzigo aliutua muda huo huo. Mwanakwetu wewe umepakata nini? Tua hilo begi weka chini ya kiti ili uweze kusafiri kwa salama na amani. Ndugu yangu saa 8 umepakata begi, angalia usivunje huo mfupa wa paja. Ukimaliza safari unafika nyumbani unachechemea unakutana na talaka juu ya meza.
Kwa leo niishie hapo, mimi
naendelea kuzaliwa pamoja na Bwana. Nakutakia sikukuu njema ya Krisimasi na
Mwaka Mpya.
0717649257
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...